Waamuzi Ally Mnyupe na Katanga Hussein Wapigwa ‘Pini’ na Bodi
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) imeendelea kuonyesha meno yake katika kusimamia nidhamu na weledi wa uamuzi nchini baada ya kuwashushia rungu waamuzi Ally Mnyupe na Katanga Hussein kwa makosa ya kuvurunda katika tafsiri ya sheria za mchezo.
Maamuzi hayo yaliyotangazwa Machi 20,2026 yamekuja kama onyo kali kwa waamuzi wote wanaochezesha ligi hiyo msimu huu, huku idadi ya waamuzi waliokwishakumbana na adhabu hiyo ikifikia 13, jambo ambalo linazidisha presha ndani ya uwanja kwa waamuzi wanaobaki msimu unapoelekea ukingoni.
Mwamuzi Katanga Hussein kutoka Tabora amejikuta akitolewa nje ya uwanja kwa mizunguko mitatu baada ya kushindwa kufanya uamuzi sahihi katika mchezo uliowakutanisha vigogo Simba na Singida Black Stars.
Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani wa hali ya juu, Katanga alishindwa kutoa adhabu ya penalti baada ya mlinda mlango wa Simba, Djibrilla Kassali, kumchezea rafu Joseph Guede wa Singida ndani ya eneo la hatari, tukio ambalo bodi imelitafsiri kama kushindwa vibaya kwa mwamuzi huyo katika kutekeleza sheria 17 za soka.
Kadhalika, rungu hilo limemfikia mwamuzi Ally Mnyupe kutoka mkoani Morogoro ambaye naye amepigwa ‘stop’ kwa mizunguko mitatu kufuatia utata uliogubika pambano la kukata na shoka kati ya Yanga na Azam FC.
Mnyupe anakumbana na adhabu hiyo baada ya macho yake kushindwa kuona tukio la penalti pale beki wa Azam, Fuentes Mendoza, alipomfanyia madhambi mshambuliaji Prince Dube wa Yanga.
Kuadhibiwa kwa wawili hawa kunaongeza idadi ya waamuzi waliofungiwa msimu huu, huku orodha hiyo ikijumuisha majina ya Tatu Malogo, Kasim Mpanga, Hamdani Said, Charles Simon, Jackson Samweli, Amina Kyando, Abdallah Bakenga, Ludovic Charles pamoja na Hussein Athuman.
Hatua hii ya bodi inalenga kurejesha imani ya klabu na mashabiki katika uchezeshaji wa haki, kwani makosa ya waamuzi yamekuwa yakidaiwa kupindua matokeo ya uwanjani na kuwanyima haki wachezaji na timu zilizojipanga vyema kwa ushindi.
Ujumbe wa bodi kwa waamuzi waliobaki uwanjani ni mmoja tu, nao ni kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu na kuepuka maamuzi ya kienyeji yanayoweza kugharimu ajira zao na heshima ya soka la Tanzania.
Wakati Mnyupe na Katanga Hussein wakianza kutumikia adhabu zao pembeni ya uwanja, macho ya wadau wa michezo sasa yapo kwa waamuzi wengine kuona kama watajifunza kutokana na makosa ya wenzao au wataendelea kuingia kwenye orodha hiyo ya aibu inayozidi kurefuka kila kukicha.

Post a Comment