'Babu' Ochoa aitwa kuziba pengo Mexico
Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Mexico, Javier Aguirre, amezua mjadala mzito katika ulimwengu wa soka baada ya kumrejesha kikosini kipa mkongwe na mhimili wa muda mrefu wa timu hiyo, Guillermo Ochoa, kwa ajili ya maandalizi ya fainali za Kombe la Dunia zinazotarajiwa kuanza Juni mwaka huu.
Ochoa, ambaye sasa ana umri wa miaka 40, anarejea kikosini kwa mara ya kwanza tangu fainali za Qatar 2022, akichukua nafasi ya kipa chaguo la kwanza, Luis Angel Malagon, aliyepata majeraha yatakayomweka nje ya michuano hiyo mikubwa itakayofanyika kwenye ardhi ya nyumbani.
Kurejea kwa kipa huyo mwenye uzoefu kunampa fursa ya kipekee ya kushiriki fainali zake za sita za Kombe la Dunia, rekodi ambayo ni adimu na ya kihistoria katika ulimwengu wa soka.
Mbali na uzoefu wa Ochoa, Aguirre amefanya mageuzi makubwa kwenye safu ya kiungo kwa kumjumuisha kwa mara ya kwanza Alvaro Fidalgo, kiungo fundi aliyezaliwa nchini Hispania lakini amepewa uraia wa Mexico mapema mwaka huu.
Fidalgo, mwenye umri wa miaka 28, amekuwa na kiwango bora tangu ajiunge na klabu ya Real Betis ya Hispania mwezi Januari, baada ya kuiongoza klabu yake ya zamani, Club America, kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Mexico mara tatu mfululizo.
Kiungo huyo anatazamwa kama mbadala sahihi wa kuziba mapengo ya wakali Edson Alvarez na Marcel Ruiz ambao wote wanauguza majeraha ya enka yaliyowapata mapema mwaka huu, huku akitarajiwa kuleta ubunifu mpya katika mfumo wa mashambulizi wa kocha Aguirre.
Katika kile kinachoonekana kama mchanganyiko wa damu changa na uzoefu, Aguirre pia amemwita kiungo kinda mwenye umri wa miaka 20, Obed Vargas, ambaye hivi karibuni amesaini mkataba wa kuitumikia miamba ya soka ya Hispania, Atletico Madrid. Vargas anatajwa kuwa mmoja wa vijana wenye vipaji vya hali ya juu nchini Mexico, na kuitwa kwake ni sehemu ya mpango wa kocha Aguirre kutengeneza safu ya kiungo yenye nguvu na kasi kuelekea michezo ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya timu ngumu za Ureno na Ubelgiji. Michezo hiyo itakuwa kipimo tosha kwa Mexico kabla ya kuanza kampeni yao ya kusaka ubingwa wa dunia mbele ya mashabiki wa nyumbani.
Ratiba ya Mexico inaonyesha kuwa itashuka dimbani Machi 28 kuikabili Ureno katika mchezo maalum wa uzinduzi wa Uwanja wa kihistoria wa Azteca uliopo Mexico City, kabla ya kusafiri hadi Chicago, Marekani, kucheza dhidi ya Ubelgiji katika Uwanja wa Soldier Field siku tatu baadaye.
Michezo hii miwili inatazamwa kama fursa pekee kwa Ochoa kuthibitisha kuwa bado ana 'makucha' ya kutosha baada ya kukaa benchi kwa muda mrefu tangu alipocheza mara ya mwisho dhidi ya Honduras mwaka 2014. Wadau wa soka nchini Mexico sasa wana shauku ya kuona kama uzoefu wa Ochoa na damu mpya ya Fidalgo na Vargas itatosha kuibeba timu hiyo katika michuano hiyo mikubwa duniani.

Post a Comment