RC MTAKA AUTAKA URAIS TOC
MKUU wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, ametangaza rasmi nia yake ya kuwania nafasi ya Urais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Aprili 12, mwaka huu. Mtaka, ambaye ana uzoefu mkubwa wa kiuongozi akiwa amewahi kuliongoza Shirikisho la Riadha Tanzania (SRT), ameweka wazi kuwa dhamira yake ni kuleta mabadiliko ya kimkakati katika michezo mingine nje ya soka.
Uamuzi wa Mtaka unakuja baada ya mchakato wa awali wa uchaguzi uliopaswa kufanyika Desemba 28 mwaka jana kufutwa na serikali. Katika mchakato huo uliositishwa, Mtaka alikuwa miongoni mwa wagombea wanne waliojitokeza kuwania kiti hicho cha juu, akichuana na Nasra Mohamed, Michael Washa, pamoja na Henry Tandau, ambaye ni Makamu wa Rais wa TOC katika uongozi unaomaliza muda wake.
Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mtaka alisisitiza kuwa anaamini ana uwezo wa kuivusha TOC kuelekea kwenye mafanikio makubwa ambayo serikali na wanamichezo wanayatarajia. Alibainisha kuwa ili michezo mbalimbali nchini ifikie kiwango cha juu cha ushindani, kuna uhitaji wa kuwa na Kamati ya Olimpiki iliyo imara na yenye maono mapana.
“Nitachukua fomu kwa sababu naamini naweza kuleta mabadiliko kwenye michezo Tanzania. Ukiacha mpira wa miguu, hii michezo mingine yote unahitaji kufika kwenye mafanikio ambayo serikali au mwanamichezo anayatarajia kwa kuwa na TOC iliyo imara,” alisema Mtaka.
Aidha, kiongozi huyo aliwapongeza viongozi waliopo madarakani kwa kazi waliyoifanya, lakini akasisitiza kuwa uchaguzi ni mchakato wa kidemokrasia unaolenga kuimarisha taasisi. Alitumia fursa hiyo kuwahamasisha Watanzania wenye sifa kujitokeza kuchukua fomu katika nafasi mbalimbali, akisema huu ni muda muafaka wa kushiriki kuleta mageuzi katika sekta ya michezo nchini.
Tayari Kamisheni ya Uchaguzi ya TOC, chini ya Mwenyekiti wake Wakili Ibrahim Mkwawa, imetoa mwongozo wa uchaguzi huo kwa mujibu wa Kifungu cha 10 cha Sheria na Kanuni za TOC, huku macho ya wanamichezo wengi yakielekezwa Aprili 12 kuona nani atapewa dhamana ya kuongoza harakati za Olimpiki nchini.

Post a Comment