RAIS SAMIA AWAPASHA WAZANDIKI: AMANI YA TANZANIA NI MSINGI USIOTIKISIKA
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa onyo kali kwa watu wasioitakia mema nchi na wanaojaribu kuchezea amani ya nchi, akisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kulinda umoja wa kitaifa na utulivu wa kisiasa kwa gharama yoyote.
Akiwasilisha msimamo huo thabiti Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, Rais Samia alibainisha kuwa utulivu wa kisiasa ndio umekuwa nguzo kuu ya maendeleo ya nchi, na serikali yake haitasita kuchukua hatua dhidi ya yeyote anayejaribu kupandikiza mbegu za chuki na farakano miongoni mwa Watanzania.
Kauli hiyo imekuja wakati akipokea salamu za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), António Guterres, zilizowasilishwa na Mjumbe Maalumu, Parfait Onanga-Anyanga, huku Rais akisisitiza kuwa Tanzania itabaki kuwa nchi inayozingatia demokrasia na utawala bora.
Katika kile kinachoonekana kama kuwajibu wazandiki wanaotumia matukio ya kisiasa kupotosha uhalisia wa nchi, Rais Samia alieleza kuwa serikali imejizatiti kuhakikisha mchakato wa kufuatilia matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea kabla na wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka jana, unafanyika kwa haki na uwajibikaji.
Alisema kuwa serikali iko tayari kupokea na kuyafanyia kazi mapendekezo ya Tume ya Uchunguzi ili kuimarisha maridhiano ya kitaifa na kuendelea na mchakato wa marekebisho ya katiba. Hatua hizi ni dhihirisho kuwa Tanzania inajiongoza kwa misingi ya sheria na si kwa shinikizo la watu wenye nia ovu wanaotaka kuona nchi ikiingia katika taharuki.
Kwa upande wake, Mjumbe Maalumu wa UN, Onanga-Anyanga, amepongeza ukomavu wa serikali ya Tanzania katika kushughulikia changamoto za kisiasa kwa njia ya mazungumzo jumuishi. Alisema kuwa Umoja wa Mataifa unatambua na kuthamini uamuzi wa Rais Samia wa kuunda Tume Huru ya Uchunguzi na dhamira yake ya kufanya mageuzi ya kikatiba, jambo linalozidi kuifanya Tanzania kuwa kioo cha amani barani Afrika.
Onanga-Anyanga alibainisha kuwa ziara yake na mashauriano aliyofanya na wadau mbalimbali, ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje, Mahakama, Bunge na vyama vya siasa, yamelenga kupata taswira halisi ya hali ya nchi na kuunga mkono juhudi za kuimarisha taasisi za kidemokrasia.
Ujumbe huo wa UN umethibitisha kuwa ulimwengu unaendelea kuitambua Tanzania kama kisiwa cha amani, licha ya jitihada za baadhi ya watu wachache kujaribu kuchafua taswira hiyo kimataifa.
Rais Samia alihitimisha kwa kutoa shukrani kwa Katibu Mkuu wa UN kwa kutuma ujumbe huo ili kusikiliza maoni ya wadau, jambo ambalo linaimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na jumuiya za kimataifa katika kukuza maendeleo jumuishi.
Msimamo huu wa serikali unatoa ujumbe mzito kwa wazandiki kuwa Tanzania iko imara, na jitihada zozote za kuivuruga nchi zitagonga mwamba mbele ya mshikamano wa dhati wa serikali na wananchi wake.
.jpeg)
Post a Comment