NI USHINDI UNAOBEBWA NA TAKWIMU KATIKA UWEKEZAJI WA MADINI, 'WAKLOROFOMU' MITANDAONI HOI
Katika kipindi ambacho baadhi ya vikundi vya 'waklorofomu' vimekuwa vikijitahidi kuamsha hisia hasi ili kuijengea Serikali picha ya kushindwa, matokeo ya utafiti wa kimataifa wa Fraser Institute 2025 yamekuja kama jibu la kisayansi linalothibitisha kuwa Tanzania sasa ni lulu ya uwekezaji.
Kupanda kwa alama za Tanzania kutoka 46.38 mwaka 2023 hadi kufikia 68.04 mwaka 2025 kwenye kielelezo cha mvuto wa uwekezaji (IAI), ni ushindi wa hoja dhidi ya kelele. Hatua hii siyo tu inaiweka Tanzania katika nafasi ya 34 duniani na ya nne Afrika, bali inawanyang’anya silaha wale wote walioaminisha umma kuwa mazingira ya biashara nchini yanayumba, ikithibitisha kuwa uaminifu wa wawekezaji wa kimataifa umerejea kwa kishindo.
Ushindi huu wa kimataifa unakwenda sambamba na mabadiliko ya mfumo wa utendaji wa ndani, ambapo Serikali imeweka wazi kuwa sasa "haidanganyiki" na maneno ya hisia bali inapima matokeo ya kidola.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 60 ya mvuto wa Tanzania unatokana na utajiri wa kijiolojia (nafasi ya 15 duniani), huku asilimia 40 ikitokana na mfumo wa sera ambao sasa unaratibiwa kwa nidhamu ya hali ya juu.
Hii inamaanisha kuwa Serikali imefanikiwa kutengeneza barabara nyeupe ya kuvutia mitaji inayofikia mabilioni ya dola kwa ajili ya utafiti na uchimbaji.
Wakati "waklorofomu" wakijaribu kupuliza maneno ya kuvunja moyo wawekezaji ili Serikali ikose mapato na ishindwe kuhudumia wananchi, takwimu zinaonyesha kuwa mwelekeo wa sasa unailinda nchi, kwani kwa kuwa katika nafasi ya nne Afrika baada ya mataifa kama Botswana na Morocco, Tanzania imetangaza kuwa iko tayari kuchuana kibiashara, huku ikihakikisha kuwa kila uwekezaji unaoingia unachochea kukuza pato la Taifa na kutengeneza ajira za kudumu kwa vijana.
Hatimaye, vita hii dhidi ya waklorofomu inashinda kwa kutumia "Dira ya 2050" kama muongozo mkuu, huku matokeo ya sekta ya madini yakiwa ni kielelezo cha kile kinachoweza kutokea katika sekta nyingine kama kukiwa na nidhamu ya kisera.
Kwa kuorodheshwa miongoni mwa maeneo bora duniani kwa mvuto wa kijiolojia, Tanzania inatuma ujumbe mmoja tu kwa ulimwengu: nchi iko mikono salama, mazingira ni rafiki, na wale wote wanaojaribu kuamsha hisia potofu ili kukwamisha maendeleo, wamezidiwa na kasi ya takwimu na ukweli wa mambo unavyoonekana uwanjani.

Post a Comment