IFTARI YA MAJALIWA YAIPIGIA SALUTI SERIKALI YA RAIS SAMIA
Katika dhihirisho la hali ya juu la umoja na mshikamano wa kitaifa, Waziri Mkuu Mstaafu, Kassim Majaliwa, ameungana na Watanzania kuipa "High Five" Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuifanya Tanzania kuwa kimbilio la amani na utulivu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam mnamo Machi 10, 2026, wakati wa hafla ya Iftari maalumu iliyowakutanisha viongozi wa dini, wanasiasa, wanahabari, na wanamichezo, Majaliwa alibainisha kuwa uhuru na utulivu unaoshuhudiwa nchini si jambo la bahati mbaya, bali ni matokeo ya usimamizi thabiti na maono ya mkuu wa nchi katika kutunza tunu za taifa.
Majaliwa, ambaye pia ni mshauri wa Rais, alitumia jukwaa hilo kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kumshukuru Rais Samia kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha jamii inakaa pamoja bila hofu, huku akilinganisha hali hiyo na mataifa mengine duniani yanayokumbwa na misukosuko.
Alisisitiza kuwa wakati mataifa mengine yakihofia kesho yao, Tanzania ina uhakika wa kesho kutokana na misingi ya amani iliyowekwa. Kauli hii ni sifa tosha kwa serikali inayojali utu na umoja, ikithibitisha kuwa uongozi wa Rais Samia umekuwa mwavuli unaowaunganisha wote bila kujali itikadi wala imani zao.
Viongozi wa dini nao hawakubaki nyuma katika kuunga mkono juhudi hizo za serikali, ambapo Majaliwa aliwapongeza kwa kuwa walinzi wa maadili na amani kila panapojitokeza viashiria vya mnyukano.
Alimtambua Shehe Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar Zubeir, na viongozi wa madhehebu mengine kama maaskofu na wachungaji kwa mchango wao mkubwa katika kujenga mshikamano. Mufti Zubeir alikazia kuwa mwezi wa Ramadhani ni shule ya tabia njema inayofundisha kuishi kwa wema na watu wote, jambo ambalo limekuwa utamaduni wa Watanzania chini ya serikali sikivu.
Hafla hiyo iliyopambwa na tabasamu na mazungumzo ya kidugu, imeacha ujumbe mzito kwa jamii kufuata maelekezo ya viongozi wa dini na kuendelea kuiunga mkono serikali katika kudumisha utulivu.
Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Omar, alihitimisha kwa kumpongeza Majaliwa , akibainisha kuwa matukio kama hayo ndiyo yanayotengeneza undugu na upendo. Ni wazi kuwa ushirikiano huu kati ya viongozi wastaafu, serikali, na taasisi za dini ndio siri inayofanya Tanzania kuendelea kung'ara kama kioo cha amani barani Afrika na duniani kote.

Post a Comment