Nyota wa Tembo Warriors Emmanuel Mlefu Atua Uturuki
Katika kile kinachoonekana kuwa ni muendelezo wa mafanikio makubwa kwa soka la walemavu nchini, mchezaji wa timu ya taifa ya Tembo Warriors, Emmanuel Mlefu, amefanikiwa kuanza ukurasa mpya wa soka la kulipwa nchini Uturuki.
Mlefu amekamilisha ndoto hiyo baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili na klabu ya Sisli Yedipete inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini humo, hatua inayozidi kuipandisha hadhi Tanzania katika ramani ya michezo duniani.
Mlefu, ambaye kwa muda mrefu amekuwa nguzo muhimu katika klabu ya Sauti Parasport ya Chang’ombe jijini Dar es Salaam, tayari amewasili nchini Uturuki na kujiunga na wenzake tayari kwa msimu mpya.
Safari ya mchezaji huyu kuelekea soka la kulipwa ilipata msukumo mkubwa kufuatia kiwango bora alichokionyesha katika mashindano ya Afrika Mashariki na Kati yaliyofanyika Burundi mwaka jana, ambapo uchezaji wake wa kipekee uliwavuta maskauti wa kimataifa na kumpatia mlango huo wa fursa.
Akizungumza kwa njia ya mtandao akiwa nchini Uturuki, Mlefu ameeleza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya jitihada na kumtanguliza Mungu, huku akiahidi kupambana ili kuthibitisha ubora wa mchezaji wa Kitanzania.
| HEKAHEKA ZA BURUNDI |
Amesema dhamira yake kuu ni kuisaidia klabu yake mpya kufikia malengo yake na wakati huo huo kuitangaza Tanzania, huku akisisitiza kuwa uamuzi wa klabu hiyo kumsajili utalipa kutokana na kiwango atakachokionyesha uwanjani.
Uhamisho wa Mlefu unafanya idadi ya wachezaji wa Tembo Warriors wanaocheza soka la kulipwa nchini Uturuki kufikia saba, jambo ambalo ni rekodi ya kipekee kwa nchi.
Mlefu anaungana na watanzania wengine ambao tayari wapo nchini humo wakipeperusha bendera ya taifa, akiwemo Shadrack Hebron anayecheza naye klabu moja, Kassim Mbarouq wa Depsas Enerj Sport, Ramadhan Chomelo anayeichezea Kahramanmaras SK, Richard Swai wa Merdin, Mudrick Mohamed wa Mersin, pamoja na Frank Ngairo anayekipiga Sakarya Spor.
Katika ujumbe wake kwa wanamichezo wanaochipukia nchini, Mlefu amewataka kutokata tamaa na badala yake waendelee kujituma kwa subira na nidhamu ya hali ya juu.
Amesema kuwa milango ya mafanikio ipo wazi kwa kila mmoja, mradi tu kuwe na malengo ya dhati na juhudi za kuyafikia, huku akiishukuru klabu yake ya zamani ya Sauti Parasport na watanzania kwa ujumla kwa kumuunga mkono katika safari yake ya kuelekea mafanikio hayo ya kimataifa.

Post a Comment