DK. NCHIMBI AFICHUA SIRI YA ASILIMIA 20 YA PATO LA TAIFA




MAKAMU wa Rais, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ametoa mwelekeo mpya wa kiuchumi nchini akibainisha kuwa sekta ya misitu, inayojumuisha ufugaji nyuki na wanyamapori, ni miongoni mwa mihimili mikuu ya taifa inayochangia takribani asilimia 20 ya Pato la Taifa (GDP).

Akizungumza wakati akifungua maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Kampeni ya Upandaji Miti kitaifa mkoani Lindi, Dk. Nchimbi ameweka wazi kuwa uhifadhi wa misitu si suala la mazingira pekee, bali ni hitaji la lazima la kiusalama, kisayansi, na ustawi wa kijamii kuelekea Dira ya 2050.

Katika uchambuzi wa kiuchumi, Tanzania inajivunia eneo la misitu lenye ukubwa wa hekta milioni 48.1, sawa na asilimia 55 ya nchi kavu. Dk. Nchimbi amefafanua kuwa rasilimali hii ni injini inayozalisha mabilioni ya fedha kupitia mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu, utalii, na biashara ya mkaa na mbao. 

Zaidi ya hapo, misitu ndiyo inayolinda nishati na viwanda kwa kuhakikisha upatikanaji wa maji ya uhakika kwa matumizi ya uzalishaji, jambo linaloifanya sekta hii kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa kijani.

Kisayansi, Makamu wa Rais ameonyesha wasiwasi juu ya kasi ya uharibifu wa misitu inayofikia hekta 469,400 kwa mwaka. Kitaalamu, uharibifu huu ni janga la kisayansi kwani unapunguza uwezo wa ardhi kufyonza hewa ya ukaa (Carbon Sink) na kuvuruga mzunguko wa maji (Hydrological Cycle). 

Amesema kuwa hekta milioni 44.7 za miombo na misitu ya mikoko milimani ni hazina ya kibayolojia inayolinda rutuba ya ardhi na kuzuia mmomonyoko, hivyo kuifanya sayansi ya uhifadhi kuwa silaha pekee dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Kijamii, Dk. Nchimbi amebainisha kuwa kampeni ya "Tanzania ya Kijani" inayolenga kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka katika kila halmashauri, ni mkakati wa kuandaa kizazi chenye nidhamu ya mazingira. Alikemea tabia za kijamii zinazokwamisha maendeleo, ikiwemo uingizaji wa mifugo hifadhini, uvamizi wa maeneo ya misitu kwa ajili ya makazi, na uchimbaji wa madini usiozingatia kanuni, mambo ambayo yanahatarisha usalama wa chakula na maji kwa vizazi vijavyo.

"Tangu kampeni hii ianze mwaka 2023, jumla ya miti milioni 113.1 imepandwa nchi nzima. Hatuna budi kumuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kushiriki katika kupanda na kutunza miti," alisema Dk. Nchimbi huku akiziagiza halmashauri zote kuhakikisha vijiji vinakuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kuzuia migogoro na kulinda vyanzo vya asili.

No comments