UBUNIFU WA VETA KIHONDA: VIJANA WANAOTUMIA TEKNOLOJIA KUKWAMUA JAMII BADALA YA TAHARUKI




Katika ulimwengu wa sasa ambapo mitandao ya kijamii imekuwa uwanja wa malumbano na wakati mwingine matusi dhidi ya juhudi za maendeleo, kundi la vijana kutoka Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Kihonda mjini Morogoro limeamua kuandika historia tofauti. 

Vijana hawa wameonyesha kuwa mazingira wezesha yaliyowekwa na serikali katika sekta ya mafunzo ya ufundi ni fursa ya dhahabu kwa kijana mzalendo kujiendeleza na kuisadia jamii yake, badala ya kupoteza muda mwingi kufarakanisha umma kupitia teknolojia. 

Hawa ndio vijana ambao taifa linawahitaji; wanaotumia akili na maarifa yao kubuni suluhu za changamoto zinazomkabili Mtanzania wa hali ya chini.

Wanafunzi hao wameibuka na ubunifu wa mfumo wa kisasa wa umwagiliaji ambao unalenga kumpunguzia mkulima mdogo gharama za uendeshaji na kumuokoa na upotezaji wa muda. 

Mfumo huu, ambao kwa sasa umefikia asilimia 65 ya hatua za majaribio, ni uthibitisho tosha kuwa teknolojia ikitumiwa vyema inaweza kuwa mkombozi wa kiuchumi. 

John Ambrose, mmoja wa vijana wabunifu waliohusika kuunda mfumo huo, anafafanua kuwa siri ya mafanikio hayo ipo katika aplikeshini ya simu inayounganishwa na kifaa maalum kilichoundwa chuoni hapo. Mkulima anajisajili na kisha anauwezo wa kuwasha au kuzima mfumo wa maji shambani kwake kwa kubofya tu simu yake ya mkononi akiwa mahali popote.

Urahisi wa mfumo huu unakwenda mbali zaidi ambapo mkulima anaweza kupanga ratiba ya umwagiliaji na kuihifadhi kwenye simu yake, kisha mfumo unajiendesha wenyewe (auto) kwa kutoa maji na kuzima kwa muda uliopangwa. 

John anabainisha kuwa lengo kuu ni kumkwamua mtu wa hali ya chini kwani mambo ni mengi na muda ni mchache, hivyo teknolojia hii inampa mkulima nafasi ya kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo wakati shamba lake likiendelea kuhudumiwa na mfumo huo wa gharama nafuu. 

Huu ni ujumbe wa wazi kwa vijana wengine nchini kuwa, badala ya kujaza kurasa za mitandao kwa kashfa, kuna nafasi kubwa ya kutumia vifaa hivyo hivyo vya kidijitali kuleta mapinduzi ya kilimo na viwanda.

Mkufunzi na mtaalamu wa teknolojia za kilimo, Valency Shirima, anayesimamia vijana hao, amesema kuwa wanatarajia kukamilisha mfumo huo ndani ya miezi miwili ijayo ili uanze kufanya kazi rasmi. 

Hatua hii ya VETA Kihonda ni fundisho kwa vijana kuwa serikali imeshatengeneza daraja la mafunzo, na kazi iliyobaki ni kwa vijana wenyewe kuvuka daraja hilo kwa vitendo na ubunifu. Ni kupitia juhudi kama hizi ndipo taifa linajengwa, jamii inastawi, na kijana anajipatia heshima na kipato chake binafsi kupitia kazi ya mikono yake na utaalamu wa kisasa.

No comments