SERIKALI NA NBC ZAUNG’ANISHA NGUVU KULEA MAWAZO YA BIASHARA KWA WANAFUNZI




WADAU wa elimu nchini wameishauri Serikali kuanzisha mifuko maalumu ya uwezeshaji na programu za ufuatiliaji (incubation hubs) kwa wanafunzi wabunifu, ili kugeuza mawazo yao ya kibiashara kuwa biashara endelevu zitakazotatua tatizo la ajira nchini.

Hoja hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam wakati wa kilele cha shindano la kitaifa la uandishi wa insha na ubunifu wa biashara kwa wanafunzi wa sekondari, mradi ulioratibiwa na Benki ya NBC kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo.

Pendekezo hilo la wadau linakuja wakati Serikali ya Awamu ya Sita ikiwa tayari imeweka msingi imara wa ulezi wa biashara kupitia taasisi kama Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na SIDO, ambazo zimekuwa zikiendesha vituo vya ulezi (Incubators) kote nchini.

Serikali pia imekuwa ikihamasisha uanzishwaji wa vituo hivi hata kwenye vyuo vikuu na sasa nguvu hiyo inahamishiwa kwenye ngazi ya sekondari ili kuibua vipaji mapema zaidi.

Akijibu hoja za wadau, Naibu Waziri  Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Rahma Kisuo, amesema Serikali itaendelea kuunga mkono majukwaa hayo kwani ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kuandaa vijana wenye uelewa mpana wa masuala ya uchumi kuanzia ngazi za chini.

"Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada hizi kwa kuwa zinachangia kwa kiasi kikubwa kuandaa kizazi chenye uelewa mpana wa masuala ya uchumi, kuanzia ubunifu wa mawazo ya biashara hadi matumizi sahihi ya taasisi za kifedha," alisisitiza Mhe. Kisuo.

Kwa upande wake, Benki ya NBC kupitia kwa Mkurugenzi wa Uendeshaji, Alelio Lowassa, imesisitiza kuwa mashindano hayo ni jukwaa la kimkakati la kuwapika wanafunzi kuwa waajiri wa kesho. 

Lowassa amebainisha kuwa benki hiyo inaona fahari kushirikiana na Serikali katika "kuboresha" mawazo ya vijana ili yaweze kufikika na taasisi za kifedha kwa ajili ya mitaji na ukuaji.

Hatua hii ya ushirikiano wa sekta binafsi na mifumo ya kiserikali ya ulezi wa biashara inatajwa kuwa mwarobaini wa kudumu wa kutengeneza fursa mpya za kiuchumi na kupunguza utegemezi wa ajira za kiofisi miongoni mwa wahitimu.


No comments