DIT NA DIRA YA 2050: MAPINDUZI YA TEKNOLOJIA YAFUNGUA MILANGO YA DUNIA KWA VIJANA WA TANZANIA




Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imepiga hatua kubwa ya kimkakati inayolenga kuiondoa Tanzania katika utegemezi wa teknolojia kutoka nje na badala yake kuwa mzalishaji na muuzaji wa ubunifu wa kitanzania katika soko la kimataifa. 

Hatua hii si tu ni utekelezaji wa mapema wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, bali ni ishara ya ukombozi wa kifikra na kiuchumi kwa vijana wa Kitanzania. 

Kupitia uimarishaji wa tafiti na uzalishaji, DIT sasa inalenga kuuza bidhaa zake nje ya mipaka ya Afrika, jambo linaloweka bayana kuwa akili na mikono ya Watanzania ina uwezo wa kushindana na mataifa yaliyoendelea duniani.

Mkuu wa DIT, Profesa Preksedis Ndomba, amebainisha kuwa mkakati huu unakwenda sambamba na kufungua fursa za kipekee kupitia ushirikiano wa kimataifa, ikiwemo makubaliano ya kihistoria na taasisi ya Council Exchange Board of Trade (CEBOT) ya nchini Marekani. 

Kwa kijana wa Kitanzania, hii ina maana kubwa; ni kufunguliwa kwa milango ya biashara, uwekezaji, na ajira zinazovuka mipaka. Kupitia Hati hiyo ya Makubaliano (MoU), DIT inajiunganisha na mtandao mpana wa makampuni ya kimataifa, hatua inayohakikisha kuwa elimu ya ufundi inayotolewa nchini inapata hadhi na viwango vinavyokubalika duniani kote.

Kiini cha mapinduzi haya kipo katika mfumo wa Mafunzo na Elimu Kulingana na Uwezo (CBET), ambao DIT imekuwa ikiutekeleza kwa mafanikio makubwa ili kuziba pengo kati ya nadharia za darasani na mahitaji halisi ya soko la ajira. 

Mfumo huu unamlenga kijana anayeweza kubuni, kutengeneza, na kuendeleza teknolojia zinazotatua changamoto za kijamii na viwanda hapa nchini. Hii inamaanisha kuwa mwanachuo wa DIT haandaliwi kuwa mtafuta ajira mwenye bahasha mkononi, bali anaandaliwa kuwa mbunifu anayeweza kujiajiri au kuajiriwa kwa urahisi popote duniani kutokana na ujuzi wake wa vitendo.

Hivyo basi, mwelekeo huu mpya wa DIT ni wito kwa Watanzania kutambua kuwa safari ya kuelekea uchumi wa viwanda na kufikia malengo ya Dira 2050 inategemea nguvu ya teknolojia na ubunifu wa ndani. 

Hatua ya kuanza kuuza teknolojia nje ya nchi ni kielelezo cha majivuno ya kizalendo yanayopaswa kuungwa mkono na kila mdau. Kwa kuwekeza katika ujuzi wa vijana na kuwapa majukwaa ya kimataifa, Tanzania inatengeneza kizazi cha wabunifu watakaoliongoza taifa kuwa kitovu cha teknolojia barani Afrika na kielelezo cha maendeleo ya kweli katika karne hii

No comments