MAGEUZI YA KIUCHUMI: SERIKALI YAMWAGIA FEDHA NA FURSA WANAWAKE ILI KUKUZA TAIFA
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhihirisha kwa vitendo kuwa ukombozi wa mwanamke kiuchumi si jambo la hiari, bali ni nguzo mama ya kukuza uchumi jumuishi na endelevu kwa taifa zima.
Katika ufunguzi wa Mkutano wa Tatu wa Wanawake katika Sekta ya Fedha (Women in Finance Conference 2026) jijini Arusha, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, amebainisha kuwa wanawake ndio injini ya uchumi wa ndani wakiongoza zaidi ya asilimia 50 ya biashara ndogo na za kati nchini.
Mafanikio ya jitihada hizi yanajidhihirisha kupitia takwimu ambazo hazidanganyi, ambapo kati ya mwaka 2022 na 2025, zaidi ya wanawake milioni 1.3 nchini wamenufaika na mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 748 kupitia mifuko mbalimbali ya uwezeshaji.
Fedha hizi zimekuwa chachu ya kuanzisha na kukuza biashara, huku sekta ya fedha ikitakiwa kupanua zaidi huduma za bima, masoko ya mitaji na mifumo ya kidijitali ili kumfikia mwanamke aliyeko nyanjani.
Kwa upande wake, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa mstari wa mbele kupitia programu maalum za mikopo na ujenzi wa miundombinu ya masoko, ikiongozwa na mlezi wa chama hicho, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, anayesisitiza ushirikiano wa wadau wote katika kuweka mazingira wezeshi.Mageuzi haya hayajaishia kwenye kutoa mikopo pekee, bali yameingia hadi kwenye ngazi za juu za maamuzi ndani ya taasisi za kifedha nchini.
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Sauda Msemo, ameweka wazi msimamo wa Benki Kuu wa kuhakikisha walau theluthi moja ya viongozi katika menejimenti na bodi za benki nchini wawe ni wanawake. Agizo hili lenye muda maalum wa utekelezaji limeanza kuzaa matunda, likilenga kuziba mapengo ya kimuundo na kuhakikisha kuwa sauti ya mwanamke inasikika pale maamuzi mazito ya kifedha yanapofanyika. Hii ni hatua ya kimkakati inayolenga kuleta ufanisi wa soko na kushughulikia vikwazo vya watumiaji wa huduma kwa usahihi na umakini.
Rais wa Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha Tanzania (TAWiFA), Bi. Fikira Ntomola, amesisitiza kuwa uwezeshaji huu ni mkakati wa msingi wa kukuza uchumi wa taifa na si jambo la hisani. TAWiFA imekuwa ikichukua hatua madhubuti kwa kutoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa mamia ya wajasiriamali mikoani Dodoma, Arusha na Zanzibar, pamoja na kuanzisha programu ya uanagenzi kwa viongozi wanawake wa baadaye.

Post a Comment