AJIRA 300 SAUDI ARABIA ZATANGAZWA: WAUGUZI WA TANZANIA KULIPWA HADI MILIONI 7 KWA MWEZI



Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) kwa kushirikiana na kampuni ya Dalba Consulting Group ya Saudi Arabia  imetangaza neema ya fursa 300 za ajira kwa wauguzi nchini Saudi Arabia. 

Fursa hizi adhimu zimetolewa na Wizara ya Afya ya Saudi Arabia kwa lengo la kuajiri wataalamu wa Kitanzania wenye sifa za ushindani katika sekta ya afya duniani.

Nafasi hizo za ajira ni matokeo ya matunda ya dhati ya Diplomasia ya Uchumi inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuimarika kwa mahusiano ya pande mbili kati ya Tanzania na nchi za Mashariki ya Kati.

Hatua hii ni kielelezo tosha cha maono ya Rais Samia katika kuhakikisha nguvu kazi ya Kitanzania inapata fursa ya kutambulika kimataifa, huku ikiongeza mnyororo wa thamani wa ujuzi na kuingiza fedha za kigeni nchini. 

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Machi 30, 2026, fursa hizi zinawalenga wauguzi wanawake wenye umri kati ya miaka 23 na 45, waliotunukiwa Shahada ya Kwanza ya Uuguzi na kuendelea. Sifa nyingine za lazima ni pamoja na kuwa na leseni hai kutoka Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC) pamoja na uzoefu wa kazi usiopungua miaka miwili, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha huduma bora zinatolewa chini ya mkataba wa miaka miwili wenye kipengele cha kuhuishwa.

Mbali na maslahi mapana ya mshahara yanayofikia hadi Shilingi 7,000,000 kwa mwezi, mwajiri amejidhatiti kugharamia mahitaji yote muhimu ya mtumishi. Hii ni pamoja na tiketi za ndege za kwenda na kurudi, malazi bora, chakula, huduma za matibabu, pamoja na usafiri wa kila siku kutoka nyumbani hadi kituo cha kazi bila gharama yoyote kwa mwajiriwa.

Wataalamu wenye sifa wanahimizwa kuchamkia fursa hii kwa kutuma wasifu wao (CV) kupitia barua pepe ya dalbatanzania@gmail.com na kukamilisha usajili wao kupitia mfumo wa ajira wa Serikali (https://jobs.kazi.go.tz). Dirisha la maombi liko wazi hadi tarehe 12 Aprili, 2026. 

Machi 27,2026  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, wakati wa hafla ya kuaga kundi la vijana 521 wanaokwenda kufanya kazi katika mataifa mbalimbali ughaibuni, 45 wakienda bara la Ulaya zikiwemo nchi za Denmark,Poland, Bosnia na Ujerumani, alitangaza kuwapo kwa neema  fani ya uuguzi nchini.  

Alisema siku hiyo kwamba kuna fursa za ajira 300 kwa ajili ya wauguzi wa Kitanzania kwenda kufanya kazi nchini Saudi Arabia.

Mhe. Sangu ameeleza kuwa fursa hizo ni matokeo ya ushirikiano wa karibu kati ya Serikali ya Tanzania na Wizara ya Afya ya nchi ya Saudi Arabia. Alibainisha kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za makusudi za Serikali ya awamu ya sita kupanua masoko ya ajira ya kimataifa kwa wataalamu wa Kitanzania, hususan katika sekta ya afya ambayo ina uhitaji mkubwa wa nguvu kazi yenye ujuzi na weledi duniani.

Waziri Sangu wakati huo alitoa wito mahususi kwa wauguzi wote wenye sifa stahiki kuchamkia fursa hiyo. Alisisitiza kuwa wataalamu wa afya wa Tanzania wana uwezo mkubwa, nidhamu, na weledi unaotambulika kimataifa, hivyo nafasi hizo zitasaidia kuongeza uzoefu wao wa kitaaluma na kuboresha kipato chao.

Tangu Julai 2025 hadi Machi 2026, takwimu zinaonyesha kuwa jumla ya Watanzania 6,246 wamefanikiwa kuunganishwa na fursa za ajira nje ya nchi kupitia mawakala binafsi 18 na jitihada za Serikali, jambo linaloashiria kukua kwa diplomasia ya uchumi ya nchi inayosimamiwa na kutekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan.


No comments