UTAFITI TCRA: Redio Yaongoza kwa Usikivu Tanzania, Runinga na Intaneti Zazidi Kuchanja Mbuga
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa matokeo ya utafiti wa hali ya utangazaji nchini kwa mwaka 2025/2026, ikionyesha kuwa redio inaendelea kuwa chanzo kikuu cha habari na burudani kwa Watanzania wengi.
Utafiti huo unabainisha kuwa asilimia 85 ya watumiaji wa huduma za utangazaji wanategemea redio, huku ikifuatiwa kwa karibu na televisheni pamoja na matumizi ya intaneti ambayo yamekua kwa kasi kubwa katika maeneo ya mijini na vijijini.
Akiwasilisha utafiti huo Injinia Andrew Kisakawa TCRA amesema upande wa Televisheni, utafiti unaonyesha kuwa asilimia 65 ya watazamaji sasa wanatumia ving'amuzi (DTT na DTH), huku maudhui ya ndani yakipendwa zaidi na asilimia 70 ya watazamaji ikilinganishwa na maudhui ya nje.
Hali hii inatoa fursa kubwa kwa wazalishaji wa maudhui nchini kuongeza ubunifu ili kukidhi mahitaji ya soko ambalo linazidi kuwa na ushindani mkubwa, hasa kutokana na kuingiliana kwa huduma za utangazaji na zile za intaneti (OTT).
Utafiti huo pia umeibua changamoto zinazowakabili watoa huduma, ikiwemo gharama za uendeshaji na mabadiliko ya tabia ya watumiaji ambao sasa wanapendelea kupata habari kupitia simu janja. Ripoti inashauri watoa huduma za kienyeji (traditional broadcasters) kuanza kuwekeza zaidi katika majukwaa ya kidijitali ili wasipitwe na wakati, kwani asilimia 45 ya vijana waliohojiwa walisema wanapata habari zao kupitia mitandao ya kijamii kabla ya kusikiliza redio au kutazama televisheni.
Kuhusu ubora wa huduma, TCRA imebaini kuwa usikivu wa redio vijijini bado unahitaji maboresho zaidi, ambapo asilimia 40 tu ya maeneo ya pembezoni yana usikivu wa uhakika wa saa 24. Mamlaka imeahidi kutumia matokeo haya ya utafiti kuboresha kanuni na sera za utangazaji nchini ili kuhakikisha kuwa sekta hii inachangia kikamilifu katika uchumi wa kidijitali na kutoa haki ya habari kwa kila Mtanzania popote alipo.
Post a Comment