MAPINDUZI YA KIDIJITALI: TCRA Yaanzisha Utangazaji wa Redio wa DSB, Yaweka Nguvu Utangazaji Vijijini
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kukamilika kwa maandalizi ya kiudhibiti na kupatikana kwa watoa huduma wa miundombinu kwa ajili ya kuanza kwa utangazaji wa redio kwa teknolojia ya kidijitali nchini, inayojulikana kama Digital Sound Broadcasting (DSB). Hatua hiyo inalenga kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani na kuongeza ubora wa huduma za utangazaji kwa wananchi.
Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Watoa Huduma za Utangazaji ulioanza leo Februari 12, 2026, katika ukumbi wa New Generation jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari amebainisha kuwa teknolojia hiyo mpya ya DSB itaanza kupatikana katika mikoa mitano ya majaribio ambayo ni Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha, na Mbeya.
Hatua hiyo inakuja wakati sekta ya utangazaji nchini ikizidi kukua, ambapo hadi kufikia Desemba 2025, TCRA imetoa jumla ya leseni 707, zikiwemo leseni 318 za maudhui mtandaoni na 258 za redio.
Mkutano wa mwaka huu umebeba kauli mbiu isemayo: “Matumizi ya Teknolojia katika Kupanua na Kuboresha Huduma za Utangazaji Vijijini,” ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa Mei 2025.
Maelekezo hayo yanahimiza kuimarisha vyombo vya habari vya jamii, vikiwemo redio jamii na televisheni ndogo za vijijini, ili kutoa fursa kwa wananchi wa maeneo hayo kunufaika na uchumi wa kidijitali.
Katika kuelekea Siku ya Redio Duniani inayoadhimishwa kesho tarehe 13 Februari, Mkurugenzi huyo amewahimiza wadau kutafakari nafasi ya Akili Unde (AI) katika utoaji wa huduma za utangazaji. Amesema kuwa TCRA kwa kushirikiana na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, inaandaa miongozo ya matumizi ya AI ili kuchochea matumizi sahihi ya teknolojia hiyo mpya katika uzalishaji na usambazaji wa maudhui nchini.
Mbali na teknolojia, TCRA imeendelea kuimarisha weledi wa wanahabari ambapo katika kipindi cha mwaka 2024 hadi 2026, jumla ya waandishi wa habari 3,125 wamepatiwa mafunzo ya kizalendo, maadili, na matumizi ya akili unde.
Aidha, Mkurugenzi huyo amegusia maandalizi ya utoaji wa Tuzo za Samia Kalamu (Samia Kalamu Award - SKA) ambazo zitatolewa kwa wanahabari na vyombo vya habari vitakavyoonyesha weledi wa hali ya juu katika kutoa huduma kwa jamii.
Kuhusu usikivu, mamlaka imeeleza kuwa usikivu wa redio nchini umefikia asilimia 85 kupitia miundombinu ya ardhini, huku televisheni kupitia satelaiti ikifikia asilimia 100. Ili kutatua changamoto ya usikivu mipakani, vituo 17 vya utangazaji vimejengwa na vingine 10 viko katika hatua za ujenzi kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), hatua itakayohakikisha kila Mtanzania anapata habari bila kikwazo cha kijiografia.
Post a Comment