SERIKALI YASHUSHA ADA ZA LESENI KWA WANABLOGU, WATOA MAUDHUI MTANDAONI
Serikali imetangaza neema ya kihistoria kwa wanablogu, vijana wabunifu, na watoa maudhui mtandaoni baada ya kupunguza ada za leseni kwa kiwango kikubwa, lengo likiwa ni kurasimisha shughuli za kidijitali na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.
Hatua hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wadau wa sekta hiyo walioeleza kuwa gharama za awali zilikuwa kikwazo kikubwa kwa ubunifu na ujasiriamali wa mtandaoni.
Kwa takaribani mwaka mzima Tanzania Bloggers Network (TBN) imekuwa na mikutano na watendaji wa serikali ikiwemo Mamlaka inayoshughulikia mawasiliano nchini ,TCRA, wakielezea vikwazo wanavyokutana navyo katika kuendesha shughuli za kublogu, moja ya shughuli muhimu katika kuwezesha mudhui ambayo yanadakwa na Akili Unde.
Taasisi hiyho iliendesha utafiti kuhusisna ana masuala ya blogu nchini Tanzania na kuja na mambo kadhaa ambayo serikali imezingatia na kuyafanyia kazi.
Katika mabadiliko hayo mapya yaliyotangazwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma, ada ya leseni kwa watoa maudhui mtandaoni imeshushwa kutoka shilingi laki tano (500,000) hadi shilingi elfu hamsini (50,000) tu. Aidha, ada ya maombi kwa kundi hilo sasa itakuwa ni shilingi elfu kumi (10,000) pekee, hatua inayolenga kuwawezesha vijana wengi zaidi kuingia katika mfumo rasmi wa utambuzi.
Mageuzi hayo pia yamegusa kundi la wakusanyaji wa maudhui mtandaoni (Online Content Aggregators), ambapo ada yao ya leseni imepunguzwa kutoka shilingi milioni moja (1,000,000) hadi shilingi laki moja (100,000) pekee.
Vilevile, ada ya maombi kwa kundi hili imewekwa kuwa shilingi elfu ishirini (20,000) tu, jambo litakaloongeza ushindani wenye tija na kuboresha ubora wa kazi zinazozalishwa na wanahabari wa kidijitali nchini.
Mbali na punguzo hilo la ada, Serikali kupitia Wizara ya Habari na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeanzisha kategoria mpya ya leseni iitwayo "Amateteur" kwa ajili ya vijana wanaochipukia katika uandaaji wa maudhui. Leseni hii inalenga kuondoa vikwazo visivyo vya lazima na kuwaruhusu vijana hao kujitambulisha rasmi na kukuza vipaji vyao huku wakizingatia maadili na sheria za nchi.
Ili kuwaimarisha zaidi kiuchumi, Serikali imeanza kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa watengeneza maudhui mtandaoni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa bora na vya kisasa vya kufanyia kazi.
Hatua hii inaenda sambamba na mkakati wa kudhibiti uharamia na wizi wa kazi mtandaoni, ambapo taasisi za COSOTA na TCRA zimeelekezwa kuandaa mpango madhubuti wa kulinda hakimiliki za wabunifu ili kuhakikisha jasho lao linawanufaisha wao wenyewe na si wajanja wachache.
Post a Comment