MKAKATI WAANIKWA UTEKELEZAJI MAPENDEKEZO TUME HAKI JINAI

 


MKAKATI wa utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai umeandaliwa na shughuli zake zimeainishwa kutekelezwa katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainabu Katimba, alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu (ACT-Wazalendo), aliyetaka kufahamu mpango wa serikali wa kutekeleza kwa ukamilifu mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.

“Serikali imeandaa mkakati wa utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai. Mkakati huo umeainisha shughuli zitakazotekelezwa katika kipindi cha muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu,” alisema.

Aidha, wizara za kisekta na taasisi za hakijinai zinatekeleza mkakati huo kupitia mipango na bajeti za kila mwaka.

Alisema Serikali imejenga mfumo wa kielektroniki (e-Maboresho) wa utoaji taarifa katika kipindi cha robo mwaka, nusu mwaka na mwaka. Kupitia mfumo huo, taasisi za hakijinai hutoa taarifa za hali ya utekelezaji wa mapendekezo ya tume.

Akijibu swali la nyongeza la mbunge huyo, Zainabu alisema Tume ya Haki Jinai ilitoa mapendekezo 333 na serikali imeanza kuyafanyia kazi.

“Miongoni mwa mapendekezo hayo hakuna linalogusa mabadiliko ya katiba kwa sababu misingi ya utekelezaji ipo katika Katiba kupitia Ibara ya 12 hadi 29,” alisema.

Alisema serikali ipo katika utekelezaji wa mapendekezo hayo kwa muda mfupi, wa kati na mrefu na imeunda mfumo rasmi wa utoaji taarifa za utekelezaji wake.

Aidha, alisema sheria mbalimbali zitaletwa bungeni Septemba kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho ili kuongeza ubora na ufanisi wake.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi alisema serikali ina utashi wa kisiasa kuhusu mchakato wa marekebisho ya katiba tangu Serikali ya Awamu ya Nne.

Alisema Ibara ya 98 ya Katiba inatambua uwepo wa mahitaji ya kijamii ya kurekebisha, kufuta au kuboresha sheria kulingana na matakwa ya wakati.

“Hata Ilani ya CCM imeeleza hilo, hivyo wakati ukifika marekebisho ya Katiba yatafanyika kwani ni ajenda yetu,” alisema.

 

 

No comments