TIMU YA CAF YAANZA UKAGUZI WA VIWANJA AFCON 2027




Timu ya wataalamu kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) inaendesha ukaguzi maalum katika mataifa ya Tanzania, Kenya, na Uganda ambayo yataandaa kwa pamoja fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) mwakani. 

Jopo hilo la wataalamu limeanza ukaguzi wake wiki hii na linatarajia kufikia tamati Jumanne ijayo, huku shirikisho hilo likiweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha miundombinu ya daraja la juu inapatikana kwa ajili ya mashindano hayo. Ukaguzi huo unajumuisha sehemu za kuchezea, viwanja vya kufanyia mazoezi, pamoja na miundombinu ya ulinzi na usalama itakayotumika wakati wa michuano.

Uchunguzi huo wa jopo la CAF unakuja sambamba na kikao cha Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo kinachotarajiwa kufanyika leo jijini Dar es Salaam. CAF itaanza ukaguzi wake Dar es Salaam kisha kuelekea Arusha na Zanzibar, maeneo ambayo yamepangwa kuwa mwenyeji wa mechi mbalimbali. 

Maeneo yatakayokaguliwa nchini Tanzania ni pamoja na Uwanja wa Benjamin Mkapa (Dar es Salaam), Uwanja wa Samia Suluhu Hassan (Arusha), pamoja na Uwanja wa New Amaan Complex na eneo la Fumba kule Zanzibar.

Kwa upande wa Kenya, wataalamu hao watakagua viwanja vya Kasarani, Nyayo, na Talanta Sports City, pamoja na viwanja vya mazoezi vya Ulinzi na Kenya Academy of Sports. Nchini Uganda, jopo hilo litatembelea miji ya Entebbe na Kampala kwa ajili ya kukagua Uwanja wa Mandela National Stadium (Namboole) na viwanja vingine vilivyotengwa kwa ajili ya mazoezi ili kuhakikisha vigezo vyote vya CAF vinafikiwa kabla ya kuanza kwa fainali hizo mwakani.

No comments