SERIKALI YAMWAGA BILIONI 25/- KUCHOCHEA UZALISHAJI DAWA NCHINI
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza mkakati mpya wa kuifanya sekta ya uzalishaji wa dawa kuwa kipaumbele cha kitaifa ili kuimarisha usalama wa afya na maendeleo ya viwanda nchini. Katika hatua hiyo, Serikali imetenga uwekezaji wa kiasi cha dola za Marekani milioni 10 kwa ajili ya kuanzisha Maabara ya Pamoja ya Dawa.
Akizungumza katika Jukwaa la Uwekezaji wa Uzalishaji wa Dawa Tanzania, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, amebainisha kuwa Serikali itaanzisha Vituo vya Uzalishaji wa Dawa (Pharmaceutical Manufacturing Hub Clusters) katika maeneo ya Mloganzila na Kibaha.
Maabara hiyo ya pamoja itahudumia vituo vyote viwili kwa kutoa huduma za upimaji wa ubora, tafiti za bio-equivalence, na msaada wa kitaalamu ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinakidhi viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO).
Waziri Mchengerwa amesisitiza kuwa Serikali itaweka mfumo wa sera utakaolinda uwekezaji wa ndani kwa kutoa kipaumbele kwenye manunuzi ya umma, kodi, na udhibiti mara tu wazalishaji watakapokidhi viwango vya kimataifa.
"Lengo si kuzuia uagizaji wa dawa kutoka nje, bali kuhakikisha kuwa uagizaji huo hauathiri ushindani wa haki wala kudhoofisha uwekezaji wa ndani unaozingatia ubora," amesema Waziri Mchengerwa.
Ili kuondoa urasimu, Serikali imeunda Kikosi Kazi cha Kuharakisha Uwekezaji wa Dawa (PIAT), kinachojumuisha viongozi kutoka sekta za afya, fedha, ardhi, na nishati ili kushughulikia vibali na leseni kwa pamoja.
Kufuatia hatua hizo, Serikali imetoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwasilisha maombi ya nia (Expression of Interest - EOI) kuwekeza katika uzalishaji wa dawa na bidhaa za afya. Tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maombi hayo ni 2 Machi 2026.
Mkakati huu unalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji na usafirishaji wa dawa katika kanda ya Afrika Mashariki na bara zima la Afrika.amesema kuwa serikali tayari imeanza kutekeleza ajenda ya kuwa na viwanda vya dawa na vifaa tiba ili kuhakikisha bidhaa hizo zinazalishwa kwa wingi na viwanda vya ndani, jambo ambalo litachochea maendeleo ya nchi.

Post a Comment