Serikali yafafanua utekelezaji Kima cha Chini cha Mshahara



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Deus Clement Sangu, amewataka  Maafisa Kazi nchini kote kuendelea kutoa elimu kwa wafanyakazi na waajiri kuhusu utekelezaji wa amri ya ongezeko la Kima cha Chini cha Mshahara kwa wastani wa asilimia 33.4 kilichotangazwa kupitia Gazeti la Serikali Oktoba 13, 2025. 

Katika tangazo hilo la serikali kupitia waziri mwenye dhamana,lilieleza kuwa Wastani wa Kima cha Chini cha Mshahara kimeongezeka kutoka Shilingi 275,060 hadi Shilingi 358,322 kuanzia Januari mosi,2026.

Katika taarifa yake kwa wanahabari Januari 16 ,2026 Waziri  Sangu, amefafanua kuwa ongezeko hilo la Kima cha Chini cha Mshahara kwa wastani wa asilimia 33.4 linatakiwa kutekelezwa kwa namna sahihi  kuepusha vurugu na kuongeza tija.

Waajiri na Wafanyakazi wa Sekta Binafsi kote nchini wametakiwa kuelewa kuwa viwango hivi vipya vimeainishwa kwa kuzingatia sekta mbalimbali, kama ilivyoelezwa bayana katika Jedwali la Pili la Amri husika. 

Sekta zilizoguswa na ongezeko hili ni pamoja na kilimo, afya, mawasiliano, usafirishaji, hoteli, madini, biashara na viwanda, shule binafsi, huduma za ulinzi binafsi, nishati, uvuvi na huduma ya baharini, michezo na utamaduni, pamoja na huduma nyinginezo. 

Sangu amesema kwamba hatua ya kuongeza kima cha chini lengo lake ni kuleta faraja na ustawi mkubwa kwa maelfu ya Watanzania wanaofanya kazi katika sekta binafsi,  kuboresha mazingira ya kazi na kuinua hali za wafanyakazi.

Amesema kutokana na umuhimu wakle katyika kuleta uhusiano bora kazini na ongezeko la tija, ni vyema wadau wote wa sekta binafsi kushirikiana kwa karibu na Maafisa Kazi pamoja na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi ili kuwepo na elimu zaidi na ushauri unaohitajika katika kipindi hiki cha mwanzo wa utekelezaji.

"Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kushirikiana na Waajiri, Wafanyakazi pamoja na Vyama vyao kuhakikisha mazingira ya kazi na hali za Wafanyakazi zinaboreshwa na kusimamiwa ipasavyo ili kukuza Tija na Ustawi wa Wafanyakazi," alisema Waziri Sangu.

Ufafanuzi huo wa serikali umetolewa wakati wafanyakazi zaidi ya 300 wa Kiwanda cha Chuma cha Lodhia kilichopo katika kata ya Themi mkoani Arusha,  wakigoma kuingia kazini wakidai kulipwa mshahara mdogo kinyume na agizo la Serikali kuhusu kima cha chini cha mshahara.

 Wafanyakazi hao wamedai kuwa bado wanapokea mshahara wa shilingi laki mbili, hali iliyosababisha kufanyika kwa mgomo huo.

Kutokana na mgomo huo, wafanyakazi wamezuia gari yoyote kuingia katika geti la kiwanda hicho hadi pale watakaposikilizwa. 

Akizungumza , Mwenyekiti wa Makampuni ya Viwanda vya Lodhia, Haruni Lodhia, amesema uongozi wa kampuni uko tayari kushughulikia malalamiko ya wafanyakazi ikiwemo suala la mishahara. 

No comments