Safari ya Kombe la Dunia U-17: Serengeti Girls Kukipiga na Botswana, Uganda na Kenya Kazi Wanayo!



RABAT, Morocco

 Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) limetangaza rasmi ratiba ya mechi za mchujo za kufuzu Kombe la Dunia la Wanawake chini ya umri wa miaka 17 (FIFA U-17 Women's World Cup 2026), ambapo timu ya taifa ya Tanzania, Serengeti Girls, itaanza kampeni yake dhidi ya Botswana.

Katika droo hiyo iliyochezeshwa Jumamosi jijini Rabat, jumla ya timu 31 zitachuana katika raundi tatu za mtoano ili kupata timu nne (4) zitakazoungana na wenyeji Morocco kwenye fainali za dunia.

Ratiba ya Tanzania (Raundi ya Kwanza)

Serengeti Girls wataanza ugenini nchini Botswana kati ya Aprili 10-12, 2026, kabla ya kurudiana hapa nyumbani kati ya Aprili 17-19, 2026.

Kama Tanzania itafanikiwa kuvuka kikwazo cha Botswana, itasonga mbele raundi ya pili ambapo itakutana na mshindi kati ya Jamhuri ya Afrika ya Kati au Afrika Kusini (Banyana Banyana). Hii inatajwa kuwa njia ngumu inayohitaji maandalizi kabambe.

Majirani wa Afrika Mashariki Wapewa Mitihani

Siyo Tanzania pekee, kwani mataifa mengine ya CECAFA pia yamepangiwa wapinzani wagumu katika Raundi ya Kwanza:

Uganda atavaana na Zimbabwe.

Kenya atapepetana na Namibia.

Rwanda atakuwa na kibarua kizito dhidi ya Zambia.

Burundi atacheza na Malawi.

Ethiopia atachuana na Sudan Kusini.

Hatua ya Pili na Tatu

Raundi ya pili itapigwa mwezi Mei, huku raundi ya tatu na ya mwisho itakayotoa washindi wanne itapigwa mwezi Julai 2026.

Ikumbukwe kuwa Tanzania ina rekodi nzuri katika mashindano haya baada ya kuwahi kufuzu fainali za Kombe la Dunia nchini India mwaka 2022, hivyo macho ya wadau wengi wa soka nchini yatakuwa kwa vijana hawa kuona kama wataweza kurudia historia hiyo.

No comments