Aliyejikusanyia milioni 100/- akiwaahidi Mali kutwaa Afcon2025 atiwa mbaroni





BAMAKO, Mali 

Jeshi la polisi nchini Mali limemtia mbaroni 'mtaalamu' wa tiba za asili aliyejikusanyia mamilioni ya shilingi kwa kudai kuwa  na uwezo wa kiroho wa kuwezesha timu ya taifa hilo, ‘The Eagles’, kutwaa ubingwa wa AFCON 2025 nchini Morocco .

Mtaalamu huyo aliyetambulika kwa jina la Karamogo Sinayogo, anadaiwa kukusanya zaidi ya Shilingi milioni 100 za Kitanzania (Euro 33,500) kutoka kwa mashabiki wenye shauku, akiwaahidi kuwa Mali ingeweka historia ya kuchukua taji hilo kwa mara ya kwanza.

Baada ya Mali kutolewa katika hatua ya robo fainali na Senegal, umati wa watu wenye hasira uliizingira nyumba ya Sinayogo jijini Bamako kabla ya polisi kuingilia kati na kumkamata. Mamlaka nchini humo zimemfungulia mashtaka ya utapeli na wizi wa kutumia hadaa.

"Ushirikina na utapeli ni kosa kisheria hapa Mali. Hata hivyo, ingekuwa vigumu kumkamata mtu huyu wakati mashindano yakiendelea kutokana na joto la hamasa ya AFCON," kilieleza chanzo kimoja cha habari .

Safari ya Mali Ilivyozimwa

Ndoto za Mali kuingia nusu fainali zilizimwa na Senegal kwa kichapo cha bao 1-0. Licha ya kuonyesha mchezo wa kishujaa, Mali walilazimika kucheza wakiwa pungufu baada ya kiungo wa Tottenham, Yves Bissouma, kuonyeshwa kadi nyekundu kabla ya mapumziko.

Bao pekee la Iliman Ndiaye katika kipindi cha kwanza lilitosha kuiondoa Mali mashindanoni. Katika mashindano haya, Mali haikufanikiwa kushinda mchezo hata mmoja ndani ya dakika 90 za kawaida, kwani ilivuka hatua ya 16 bora dhidi ya Tunisia kwa njia ya mikwaju ya penalti.

Kauli ya Kocha

Akizungumza baada ya mchezo huo, kocha wa Mali, Tom Saintfiet, aliwasifu wachezaji wake kwa kupambana kiume licha ya changamoto ya kadi nyekundu katika michezo miwili mfululizo.

"Tulicheza sehemu kubwa ya mchezo tukiwa na wachezaji kumi, lakini hiyo haiondoi ukweli kwamba vijana wangu walicheza kwa ujasiri mkubwa. Najivunia kiwango walichoonyesha si tu leo, bali katika mashindano yote," alisema Saintfiet.

No comments