MAKONDA ANZA KAZI KWA KISHINDO: AFUNGUA MLANGO WA MIKOPO KWA VIJANA, ATANGAZA ‘KUFUNGA MKANDA’ WIZARANI
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, ameingia rasmi ofisini leo Januari 13, 2026, kwa kishindo baada ya kutangaza mapinduzi makubwa yanayolenga kuwawezesha vijana waliojiajiri kwenye tasnia ya habari, huku akiwataka watendaji wa Wizara hiyo kujiandaa kwa kasi mpya ya utendaji.
Mhe. Makonda ametoa kauli hizo jijini Dodoma mara baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Ikulu ya Chamwino, na kufuatiwa na hafla ya makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Prof. Palamagamba Kabudi.
Neema kwa Wanahabari wa Kidijitali
Katika hatua iliyoleta matumaini mapya kwa vijana, Mhe. Makonda amesema dhamira yake ni kumuomba Mheshimiwa Rais kiasi cha Shilingi Bilioni 2 kwa ajili ya kuanzisha mfuko wa mikopo ya vifaa vya kisasa kwa vijana waliojiajiri kwenye habari na mitandao ya kijamii.
“Tunataka vijana wanaofanya kazi za habari na maudhui mtandaoni wawe na vifaa bora. Nitamuomba Mheshimiwa Rais atupatie bilioni mbili ili ziweze kuwakopesha vijana hawa wapate kamera na vifaa vya kisasa kuboresha kazi zao,” alisema Makonda.
Aidha, alitangaza mpango wa kuanzisha kitengo maalum cha mawasiliano kitakachotafsiri habari za Kiswahili kwenda lugha mbalimbali za kigeni ili kuitangaza Tanzania na fursa zake duniani kote.
Ujumbe kwa Watendaji: “Fungeni Mkanda”
Akizungumza na watendaji wa Idara na Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo, Waziri Makonda amewataka watumishi kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake waongeze kasi, weledi na nidhamu.
“Naomba kila mtendaji akae kwenye nafasi yake, aenee kwenye kiti chake na afunge mkanda vizuri. Huu ni wakati wa kufanya kazi kwa matokeo. Wananchi wanatarajia kuona mabadiliko halisi, siyo ahadi za kwenye makaratasi,” alisisitiza Makonda.
Aahidi Kulinda Alama ya Prof. Kabudi
Licha ya kuja na kasi mpya, Makonda ameweka wazi msimamo wake wa kuheshimu kazi zilizofanywa na mtangulizi wake, Profesa Palamagamba Kabudi. Amesema hatokuja na mfumo wa kubomoa, bali kujenga juu ya misingi imara iliyoachwa.
“Nimeweka msimamo wa kutobeza kazi za watangulizi wangu. Ninalinda na kuendeleza kila walichokifanya ili kwa pamoja tuache historia njema ya uongozi unaojenga. Hakuna hata jambo moja lililoanzishwa na Waziri Prof. Kabudi litakaloachwa bila kutekelezwa,” alibainisha.
Shukrani na Maono
Mhe. Makonda amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumwamini na kumpa dhamana hiyo kubwa, huku akizishukuru mamlaka mbalimbali na viongozi wa dini kwa maombi na ushauri wao.
Amewataka watendaji kuwa na mshikamano, akibainisha kuwa Wizara ya Habari ni kioo cha nchi na ndiyo injini ya kuitangaza lugha ya Kiswahili, utamaduni na vipaji vya vijana wa Kitanzania kimataifa.

Post a Comment