CAF YASOGEZA MBELE WAFCON, TWIGA KUENDELEA NA MAANDALIZI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limesogeza mbele Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON 2026) iliyokuwa ifanyike kuanzia Machi 17, 2026 nchini Morocco.
Akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa kawaida wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) uliofanyika Kahama, mkoani Shinyanga Rais wa TFF, Wallace Karia, amesema taarifa ya kuahirishwa kwa michuano hiyo ameipokea kutoka CAF juzi na kusema ratiba mpya itatangazwa baadaye.
Karia alisema uamuzi wa CAF unatokana na wenyeji wa mashindano hayo kuomba yasogezwe mbele ili kupisha upepo wa Afcon 2025 upite.
Taarifa hiyo imekuja wakati maandalizi ya timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania, Twiga Stars,yakiwa yanaendelea kujiandaa na michuano hiyo na ilikuwa imeweka kambi nchini Misri.
"Timu yetu imekuwa kwenye maandalizi ya muda mrefu na tayari ipo kwenye mashindano ya kimataifa jijini Dubai. Licha ya kuahirishwa kwa WAFCON, programu ya maandalizi itaendelea ili kuhakikisha wachezaji wanakuwa kwenye kiwango bora," alisema Karia.
Alisema Twiga Stars ilianza kambi ya maandalizi mjini Ismailia, Misri, kabla ya kusafiri hadi Dubai, Falme za Kiarabu, ambako inaendelea na michuano maalum ya iliyoandaliwa na FIFA yaliyoanza Februari 27 yakishirikisha mataifa manne, Tanzania, Ghana, Russia na Hong Kong
Post a Comment