Rais Samia Apangia Mabalozi Vituo vya Kazi



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassan, amefanya uhamisho na kuwapangia vituo vipya vya kazi mabalozi kadhaa wanaoiwakilisha nchi katika mataifa mbalimbali duniani. 

Taarifa hiyo iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Daktari Moses Kusiluka, inaonesha kuwa mabadiliko hayo yanalenga kuimarisha diplomasia ya Tanzania kimataifa na kuhakikisha utendaji wenye tija katika ofisi hizo za ubalozi.

Katika mabadiliko hayo, Balozi Togolani Edriss Mavura ameteuliwa kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa jijini New York nchini Marekani. 

Wakati huo huo, Balozi Mhandisi Cyprian John Luhemeja amepangiwa kwenda nchini Zambia wakati Balozi Salim Othman Hamad amepangiwa kuiwakilisha nchi nchini Comoro.

Mabadiliko hayo pia yamemgusa Balozi Maulidah Bwanakheri Hassan ambaye sasa amepangiwa kituo cha kazi nchini Oman, huku Balozi Daktari Suleiman Haji Suleiman akielekezwa kwenda nchini China. Aidha, Balozi Luteni Jenerali Mathew Edward Mkingule amepangiwa kuwa Balozi nchini Cuba ili kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Kwa upande mwingine, Balozi Swahiba Habib Mndeme amepangiwa kituo cha kazi nchini Sweden huku naye Balozi Musa Haji Ali akiteuliwa kuwa Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa kule New York. 


No comments