TFF YAPITISHA BAJETI YA SH BILIONI 56, KUSAKA HESHIMA AFCON 2027



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeonyesha dhamira ya dhati ya kuandika historia mpya barani Afrika baada ya Mkutano Mkuu wa 20 ulioketi mjini Kahama kupitisha bajeti ya shilingi Bilioni 56.6 kwa ajili ya mwaka wa fedha 2026. 

Bajeti hiyo, ambayo ni ongezeko kidogo kulinganisha na shilingi bilioni 56.3 ya mwaka uliopita, inatajwa kuwa muhimili mkuu wa maandalizi ya kuelekea fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) ambazo Tanzania itakuwa mwenyeji kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.

Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Mipango ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani, amebainisha kuwa vyanzo vikuu vya mapato hayo ni pamoja na ruzuku kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Shirikisho la Afrika (CAF), pamoja na vyanzo vya ndani vikiwemo viingilio, haki za matangazo, na udhamini. 

Katika mgawanyo wa matumizi, TFF inakadiria kutumia shilingi bilioni 56.4, hatua inayotarajiwa kuacha bakaa ya shilingi milioni 204, huku Rais wa TFF, Wallace Karia akijivunia kupata "hati safi" katika ukaguzi wa hesabu uliopita, jambo linaloweka mazingira ya uaminifu kwa wafadhili na serikali.

Uimara huu wa kifedha unakwenda sambamba na mkakati mzito wa Serikali na TFF katika kuandaa fainali bora zaidi za AFCON kuwahi kutokea. 






Akihutubia mkutano huo, Rais Wallace Karia amesisitiza kuwa ushirikiano na Serikali umechochea kasi ya ujenzi wa miundombinu ya kisasa katika mikoa ya Arusha, Dodoma, na maeneo ya Fumba na Kizimkazi kule Zanzibar. Karia amebainisha kuwa lengo si tu kuandaa mashindano, bali kuhakikisha timu ya taifa, Taifa Stars, inafanya vizuri na kubakiza ubingwa nyumbani, ikizingatiwa kuwa kocha sasa anapata muda wa kutosha wa maandalizi tofauti na michuano iliyopita.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ameupongeza uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza chachu ya ushindani kupitia "Goli la Mama". 

Mhita amesema motisha hiyo ya fedha kwa kila goli linalofungwa katika michuano ya kimataifa imejenga nidhamu na morali kubwa kwa wachezaji, jambo linaloonekana kuwa sehemu ya uwekezaji wa makusudi wa serikali katika kuimarisha sekta ya michezo. 

Maandalizi haya ya AFCON 2027 yanatazamwa kama fursa adhimu ya kuitangaza Tanzania, ambapo Rais Karia amewahakikishia wageni kuwa fainali hizo hazitakuwa za uwanjani pekee, bali ni nafasi ya kujionea vivutio vya utalii nchini. 

Kwa kupitishwa kwa bajeti hii na usimamizi madhubuti wa miundombinu, TFF na Serikali sasa zinafungua ukurasa mpya wa mageuzi ya soka yatakayoiacha Tanzania ikiwa na rekodi ya kipekee ya uandaaji na ushindani katika ngazi ya kimataifa.

No comments