AFCON 2027: SERIKALI YAITAKA SEKTA BINAFSI KUKUNJUA MSULI KUTEKA FURSA ZA MATRILIONI



WAKATI hamu ya wapenzi wa soka barani Afrika ikielekezwa katika michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), Serikali ya Tanzania imetupa karata yake ya kwanza kwa sekta binafsi, ikitaka wafanyabiashara wa ndani kuwa mstari wa mbele kuchangamkia fursa zitakazotokana na mashindano hayo makubwa.

Hatua hiyo imebainishwa kufuatia kikao muhimu cha Kamati Ndogo ya Maandalizi ya AFCON kilichofanyika jijini Dar es Salaam, kati ya Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma (Mwana FA), na uongozi wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), ukiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wake, Deogratius Masawe.

Tanzania, kwa mara ya kwanza katika historia, itakuwa mwenyeji wa mashindano hayo kwa ushirikiano na majirani zake Kenya na Uganda (Pamoja Bid). 

Kwa mujibu wa vyanzo kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), michuano ya AFCON imekuwa ikivuta watazamaji zaidi ya bilioni 1 duniani kote kupitia televisheni, huku maelfu ya mashabiki wakitarajiwa kumiminika nchini.

Mhe. Mwinjuma amesisitiza kuwa AFCON si soka pekee, bali ni biashara. Sekta ya utalii, usafirishaji, malazi (hoteli), na vyakula zinatarajiwa kupata neema ya kipekee. Takwimu kutoka kwa waandaaji wa AFCON iliyopita nchini Ivory Coast (2023) zinaonyesha kuwa nchi hiyo ilipata ongezeko kubwa la mapato ya ndani kutokana na wageni zaidi ya milioni 1.5 walioingia nchini humo.

Ili kukidhi vigezo vya CAF, Tanzania tayari imeanza maboresho makubwa ya viwanja vyake. Uwanja wa Benjamin Mkapa (Dar es Salaam) unaendelea na ukarabati, huku ujenzi wa uwanja mpya wa kisasa wa Samia Suluhu Hassan (Arusha) wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 30,000 ukiwa umeanza.

"Lengo letu ni kuhakikisha huduma zote zinazotolewa kwa wageni na wachezaji zinatoka kwa watanzania. Hatutaki kampuni za nje zije kuchukua fursa ambazo sekta yetu binafsi inaweza kuzifanya," alisisitiza Mhe. Mwinjuma wakati wa kikao hicho.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa TPSF, Deogratius Masawe, amesema sekta binafsi imejipanga kuwekeza kwenye miundombinu ya muda mfupi na huduma za kidijitali ili kurahisisha mawasiliano na malipo kwa wageni. Aidha, amewahimiza wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs) kuanza kuandaa bidhaa za sanaa na nguo zenye chapa ya Tanzania ili kunufaika na soko la mashabiki.


No comments