KAHAMA KUWA KITOVU CHA VIPAJI: TFF NA SERIKALI KUJENGA AKADEMI BUZWAGI




Mkoa wa Shinyanga unatarajiwa kuwa kitovu kipya cha uzalishaji wa vipaji vya soka nchini kufuatia makubaliano ya ujenzi wa kituo cha michezo (Sports Complex) katika Wilaya ya Kahama. 

Mpango huo wa kimkakati umepigiwa mstari na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kawaida wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) uliofanyika katika ukumbi wa Malex, mjini Kahama Februari 27.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Mhita ameipongeza TFF kwa uamuzi wake wa kishujaa wa kuanzisha kituo hicho katika eneo la Buzwagi, hatua itakayosaidia kuibua na kukuza vipaji vya vijana mkoani humo na Kanda ya Ziwa kwa ujumla.

 "Naipongeza Serikali kwa kushirikiana na TFF kwa jinsi wanavyoleta mapinduzi ya soka nchini. Kipekee naishukuru TFF kwa kukubali kujenga kituo hiki Buzwagi; nawaahidi ushirikiano wa kutosha kutoka mkoani na Halmashauri ya Kahama," alisema Mhita, huku akibainisha kuwa eneo hilo tayari lina miundombinu muhimu ikiwemo huduma ya maji ya uhakika.






Kwa upande wake, Rais wa TFF, Wallace Karia, ameeleza kuwa uamuzi wa kuchagua eneo hilo umetokana na uwepo wa miundombinu ya awali kama viwanja na majengo, jambo litakalopunguza kwa kiasi kikubwa gharama za ujenzi kulinganisha na miradi mingine ambapo shirikisho linaanza kila kitu kutoka chini. Karia amesisitiza kuwa mradi wa Kahama tayari umeingizwa kwenye mpango wa maendeleo wa TFF kwa lengo la kuwahudumia vijana wa Kanda ya Ziwa.

"Kituo cha Kahama kimeturahisishia kazi kwa sababu kuna majengo na uwanja tayari. Katika eneo lililobaki, tutaongeza viwanja vingine ili kukamilisha vigezo vya kituo cha kisasa cha michezo," alifafanua Karia, huku akiongeza kuwa kituo hicho kinakwenda kuwa mhimili wa tatu wa malezi ya soka nchini chini ya TFF.

Mradi huu wa Kahama unakuja kuungana na vituo vingine viwili vinavyomilikiwa na shirikisho hilo, ambavyo ni Kituo cha Kigamboni (Dar es Salaam) na Kituo cha Mnyanjani kilichopo mkoani Tanga. 

Karia alibainisha kuwa Kituo cha Tanga kimeendelea kupata hadhi ya juu na sasa kinatambulika rasmi kama Tanga FIFA Akademi, hatua inayotoa matumaini kuwa hata kituo cha Kahama kitafikia viwango vya kimataifa na kuwa chimbuko la nyota wapya wa Taifa Stars.

No comments