MKUTANO MKUU WA 20 WA TFF: MAFANIKIO NA MAONO YA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

 



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linafanya Mkutano Mkuu wake wa 20 katika Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, tukio ambalo ni kielelezo cha mabadiliko na ukuaji wa soka nchini. 

Mkutano huu unafanyika tarehe 28 Februari 2026 katika ukumbi wa Malex Hall ukiwakutanisha wajumbe 87 na wadau zaidi ya 600 kujadili mustakabali wa mchezo huu. 

Katika mkutano huu, wajumbe wanatarajiwa kuibua fursa mpya za maendeleo, kujadili changamoto zinazoukabili mchezo huo na kufanya uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi ya mjumbe wa kamati ya utendaji Kanda namba moja baada ya kujiuzulu kwa Hosea Lugano.

Katika kipindi cha mwaka 2025, TFF chini ya uongozi wa Rais Wallace Karia imepata mafanikio makubwa yaliyoimarisha hadhi ya Tanzania kimataifa.

Ligi Kuu ya NBC imeendelea kung'ara kwa kushika nafasi ya sita kwa ubora barani Afrika, huku kukiwa na ongezeko kubwa la wadhamini na uwekezaji katika miundombinu ya klabu kama vile viwanja vya Azam, Namungo na KMC. Aidha, shirikisho limefanikiwa kupata Hati Safi ya ukaguzi wa hesabu kwa mwaka 2024, jambo linaloonyesha ukomavu katika usimamizi wa rasilimali na fedha za umma na wadau.

Maendeleo ya soka la vijana na wanawake yamekuwa kipaumbele cha kipekee kupitia programu ya FIFA ya kuendeleza vipaji (TDS) inayojumuisha vijana kuanzia miaka 13 hadi 17 nchi nzima. 

Mafanikio mengine ya kihistoria ni ushiriki wa Timu ya Taifa ya Futsal kwa Wanawake katika Fainali za Kombe la Dunia nchini Philippines, ambapo Tanzania ilionyesha ushindani mkubwa. Pia, kwa mara ya kwanza, Tanzania imeingia katika ulimwengu wa michezo ya kielektroniki (eFootball) kwa kushiriki mashindano ya kufuzu kanda ya Afrika, hatua inayofungua milango kwa vijana wengi zaidi.

Fikira na maono ya TFF yamejikita katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa mwaka 2023-2027 unaolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha soka barani Afrika. 

Shirikisho linanuia kuendelea kuimarisha utawala bora, uadilifu katika michezo na kupambana na upangaji wa matokeo kupitia elimu na teknolojia. Vilevile, kuna mkakati thabiti wa kuongeza mapato kupitia masoko na ushirikiano na taasisi mbalimbali kama TRA na NBAA ili kuhakikisha vilabu vinaendeshwa kitalaamu na kuwa na hesabu zinazokubalika kimataifa.

Mkutano huu wa Kahama unalenga kuacha alama ya maendeleo kwa mkoa wa Shinyanga na nchi kwa ujumla kwa kuhakikisha kila mdau anashiriki katika kuleta ufumbuzi wa changamoto zilizopo. 

Maono ya "Kazi na Utu" yanaendelea kuongoza harakati za kukuza vipaji kuanzia ngazi ya chini mpaka timu za taifa, huku lengo likiwa ni kuendelea kupanda katika viwango vya FIFA na CAF. 

Kwa kufanya mkutano huu nje ya makao makuu, TFF inadhihirisha nia yake ya kupeleka fursa za mpira wa miguu katika kila kona ya Tanzania.


No comments