MPOGOLO AWASILISHA MAFANIKIO YA ILANI ILALA: MADARASA MAPYA KWA WANAFUNZI 65,000 KUJENGWA
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha kuanzia Desemba 2025 hadi Februari 2026, akibainisha hatua kubwa zilizopigwa katika sekta za kijamii na kiuchumi.
Akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Ilala, Mpogolo amesema kuwa kipaumbele kikubwa kwa sasa ni sekta ya elimu ambapo Halmashauri imetenga fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vitakavyopokea wanafunzi 65,000 ili kutatua changamoto ya msongamano mashuleni.
Katika ripoti yake, Mpogolo amebainisha kuwa miradi ya maendeleo ndani ya wilaya hiyo imekamilika kwa wastani wa asilimia 89, huku akisisitiza kuwa nguvu kubwa inaelekezwa kumalizia changamoto zilizosalia kwenye sekta ya miundombinu ya elimu. Aidha, ametoa agizo kwa viongozi wa ngazi ya kata kusimamia kwa ukaribu utoaji na urejeshaji wa mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri kwa makundi ya wanawake, vijana, na wenye ulemavu, akitaka ushirikiano wa karibu na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) katika kuratibu vikundi hivyo.
Kuhusu kero za wananchi, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka viongozi wa chama na Serikali kushirikiana kwa dhati katika kutatua migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiwakabili wakazi wa Ilala kwa muda mrefu.
Mpogolo ametumia fursa hiyo kuwapongeza madiwani, wabunge, na wajumbe wa Halmashauri Kuu kwa ushirikiano wao uliowezesha miradi mingi kutekelezeka, huku akitangaza kuwa wenyeviti wa Serikali za mitaa 159 ndani ya wilaya hiyo wanatarajia kukabidhiwa vitambulisho vyao vya kazi hivi karibuni baada ya taratibu zote kukamilika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Sidde, amempongeza Mkuu wa Wilaya pamoja na Katibu Tawala, Charangwa Selemani, kwa usimamizi mzuri wa shughuli za maendeleo.
Mwenyekiti Sidde amesema kuwa siri ya mafanikio ya Ilala inatokana na mahusiano imara yaliyopo kati ya chama na Serikali, ambapo pande zote mbili zimekuwa zikishirikiana kwa karibu katika kuhakikisha ahadi zilizotolewa kwa wananchi zinatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.

Post a Comment