Mwandishi aiomba CAF inyang’anye Kenya, Tanzania na Uganda Uenyeji AFCON 2027

 


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF), Patrice Motsepe, amelazimika kutoa kauli madhubuti kufuatia ombi la kutaka uenyeji wa Mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 uhamishwe kutoka Afrika Mashariki.

Kenya, Uganda, na Tanzania zinatarajiwa kuandaa mashindano hayo mwakani chini ya mwavuli wa "Pamoja Bid," lakini mataifa hayo yameshutumiwa kukosa miundombinu inayokidhi vigezo.

Hali hiyo imejitokeza huku fainali ya AFCON 2025 ikitarajiwa kupigwa Jumapili jioni jijini Rabat kati ya mabingwa watetezi Senegal na wenyeji Morocco.

Kauli ya Mwandishi Yaibua Taharuki

Mwandishi wa habari kutoka Ivory Coast, Mamadou Gaye, amezua mjadala mzito na hasira mitandaoni baada ya kuiomba CAF kuinyang’anya Afrika Mashariki haki ya kuandaa AFCON 2027. 

Akizungumza mbele ya Rais Motsepe wakati wa mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumamosi, Gaye aliponda hali ya miundombinu katika nchi hizo tatu, akidai kuwa hazina barabara za kutosha na inaweza kuchukua hadi "siku mbili" kusafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine.

"Mashindano yajayo yanakwenda katika nchi tatu za Afrika Mashariki ambazo nimeshawahi kuzitembelea. Hakuna barabara katika nchi hizo. Baadhi ya wenzangu kutoka huko waliniambia inaweza kukuchukua siku mbili kusafiri kwa barabara," alisema Gaye.

Mwandishi huyo aliongeza kuwa wasiwasi wake mkubwa ni kwamba kiwango cha AFCON kitashuka ikiwa mashindano hayo yatafanyika Afrika Mashariki. Alitolea mfano Guinea ilivyonyang'anywa uenyeji na kupewa Morocco, na kuhoji ikiwa kuna uwezekano wa AFCON 2027 kuhamishwa au kuahirishwa.

Mashabiki Walipuka kwa Hasira

Mashabiki wa soka mitandaoni wamejibu mapigo wakitaja kauli hiyo kuwa ni ya dharau kwa ukanda wa Afrika Mashariki.

Sirmoi Wekesa aliandika: "Swali la kijinga sana. Mwache asafiri kuja Afrika Mashariki, atashtushwa na uwekezaji uliopitiliza katika miundombinu."

Captain Fish alieleza: "Kenya iko mbali sana kimaendeleo ya miundombinu kuliko nchi nyingi za Afrika Magharibi ambazo zimeandaa mashindano haya kwa miaka mingi."

Trav naye alichangia: "Huyu ni Mwafrika mwenzetu mwenye mtazamo huu kuhusu bara lake, kisha anatarajia wageni watuone tofauti? Ukweli ni kwamba Ivory Coast haijaendelea kulinganisha na miji ya Afrika Mashariki."

Motsepe Aziba Watu Midomo

Rais Motsepe alimjibu mwandishi huyo papo hapo, akisisitiza kuwa ana wajibu wa kuendeleza mpira wa miguu barani kote na si katika nchi chache tu.

"Nina wajibu wa kuendeleza mpira wa miguu kote Afrika. Siwezi kuwa na mpira kwenye nchi zenye miundombinu bora pekee, lakini nina imani kuwa AFCON ya Kenya, Uganda, na Tanzania itakuwa na mafanikio makubwa sana. Hatutaiondoa michuano hiyo katika nchi hizo," alisema Motsepe kwa msisitizo.

No comments