Muigizaji Michelle Yeoh Ang’ara Kwenye Tuzo za wazinguaji 2026: Snow White Yakamata Mkia
Miaka mitatu tu tangu anyakuwe Oscar, Michelle Yeoh sasa anachuana na akina Natalie Portman na Ariana DeBose kuwania tuzo ambayo hakuna mwigizaji anayetaka kuitwa jukwaani kuipokea.
Waandaaji wa Tuzo za Golden Raspberry (Razzies) mnamo Jumatano walimwaga hadharani orodha ya filamu na waigizaji "waliozingua" zaidi mwaka jana. Badala ya kusifu ufundi, Razzies inatoa tuzo za kufanya vibaya katika uhusika.
Katika upande wa waliofeli vibaya zaidi, filamu ya Disney, Snow White, imeongoza jahazi kwa kuteuliwa kama filamu mbaya zaidi na toleo la hovyo zaidi (remake). Filamu hiyo ya mwaka 2025 imemfanya mwongozaji Mark Webb aingie kwenye orodha ya "walioboronga," huku "Vibwengo Saba wa Bandia" wakiteuliwa kama washiriki walioharibu zaidi picha.
Sherehe hizi za 46 za Razzies zitatoa hukumu yake Machi 14, siku moja kabla ya lile shindano la kifahari la Oscar. Mshindi wa "tuzo" hii ya Razzies hupewa kikombe cha shaba iliyopuliziwa rangi ya dhahabu ya bei nafuu na kuachiwa doa la aibu kwenye rekodi yake.
Snow White itabidi "ichuane" na filamu kama The Electric State na Star Trek: Section 31 ili kuamua nani aliyepwaya zaidi. Mpaka sasa, Snow White na War of the Worlds zimefungana kwa kuwa na madongo mengi zaidi—kila moja imepata uteuzi mara sita.
Kwenye upande wa wanaume waliofunika kwa ubovu, mshindi wa zamani wa Oscar Jared Leto anaongoza jahazi. Anachuana na majina makubwa kama Scott Eastwood, bondia Dave Bautista, na wasanii wa muziki Ice Cube na The Weeknd ambao wamejikuta kwenye vita wasiyoipenda.
Kwa upande wa wanawake, ushindani ni mkali kati ya mastaa wa Oscar: Natalie Portman, Ariana DeBose, na Michelle Yeoh. Wote hawa wanashikishwa adabu kwa "kuigiza chini ya kiwango" na wanachuana na akina Rebel Wilson na Milla Jovovich.
Mkongwe Sylvester Stallone, ambaye tayari ana makombe 12 ya Razzies kabatini, amerudi tena kuteuliwa mwigizaji msaidizi mbaya zaidi, huku binti yake Scarlet Rose Stallone akifuata nyayo za baba yake kwa kuteuliwa upande wa wanawake.
Hata nguli Robert De Niro hajapona; kamati imesema alicheza wahusika wawili kwa mpigo lakini wote akawacheza "hovyo" kwenye filamu ya Alto Knights.
Post a Comment