DKT. MWIGULU AZINDUA MELI MV NEW MWANZA, ATANGAZA VITA DHIDI YA MATUMIZI YA FEDHA KWA MAZOEA
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amezitaka Wizara, Taasisi za Serikali, na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuacha mara moja utendaji kazi wa mazoea na badala yake kuelekeza rasilimali fedha katika kukamilisha miradi ya maendeleo inayowagusa wananchi moja kwa moja.
Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo leo Ijumaa, Januari 23, 2026, jijini Mwanza, wakati akizungumza na maelfu ya wananchi katika hafla ya uzinduzi wa meli ya kisasa ya MV New Mwanza (Hapa Kazi Tu), katika Bandari ya Mwanza Kusini.
Agizo kwa Wizara na Wakandarasi Katika hotuba yake, Waziri Mkuu ameelekeza wizara za kisekta kufanya tathmini ya haraka ya miradi yote ambayo utekelezaji wake umesua-sua kutokana na wakandarasi kutolipwa fedha za awali. Ameagiza kufanyika kwa mapitio ya matumizi yote yasiyo ya lazima ili fedha hizo zielekezwe kwenye miradi ya kipaumbele.
"Fedha ndogo ndogo tunazozitumia kwa mazoea ndizo zinaweza kumaliza miradi iliyosimama. Ni lazima tubadilishe mtazamo na kuweka kipaumbele kwenye mahitaji halisi ya wananchi," alisisitiza Dkt. Mwigulu, huku akibainisha kuwa mafungu ya ulinzi, usalama, na afya yasiguse kabisa katika mpango huo wa kubana matumizi.
Mv New Mwanza: Mapinduzi ya Usafiri Majini Akizungumzia meli hiyo mpya, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema kukamilika kwa MV New Mwanza ni matokeo ya dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita. Alibainisha kuwa mradi huo uliogharimu Shilingi Bilioni 120.56, ulikuta ukiwa katika hatua ya asilimia 40 pekee, lakini Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa fedha zote zilizosalia ili kuhakikisha unakamilika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli (TASHICO), Eric Hamisi, ameeleza kuwa MV New Mwanza ndiyo meli kubwa zaidi katika Ukanda wa Maziwa Makuu na Barani Afrika. Meli hiyo yenye urefu wa mita 92.6 ina uwezo wa kubeba:
Abiria: 1,200.
Mizigo: Tani 400.
Magari: Magari madogo 20 na makubwa 3.
Muda wa Safari: Saa 6 hadi 7 (Mwanza - Bukoba).
Usalama na Miundombinu Mingine Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu pia ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa miundombinu ya kusukuma na kuhifadhi maji mkoani Mwanza, pamoja na kuzindua Kituo cha Kikanda cha Kuratibu Uokoaji Majini (Search and Rescue) kilichogharimu Shilingi Bilioni 19.8. Amesema kituo hicho ni lazima kifanye kazi saa 24 ili kuhakikisha usalama wa abiria na vyombo vyote ndani ya Ziwa Victoria.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, ameishukuru Serikali kwa miradi hiyo, akisema ni mkombozi mkubwa kwa uchumi wa wana-Mwanza na kanda nzima ya ziwa, kwani inakwenda kutatua kero za muda mrefu za usafiri na huduma za maji safi.
Post a Comment