China Yaahidi Kuendeleza Ushirikiano wa Kimkakati na Tanzania
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imeeleza utayari wake wa kuendelea kuisaidia Tanzania katika juhudi zake za maendeleo, huku mataifa hayo mawili yakikubaliana kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
Hatua hiyo imefikiwa jijini Dar es Salaam wakati wa mazungumzo ya pande mbili kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Mhe. Wang Yi, na mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Wang Yi alisisitiza kuwa China itaendelea kuwa mshirika wa kuaminika wa Tanzania na Afrika nzima katika kutekeleza ajenda za maendeleo ya pamoja. Alibainisha kuwa utayari huo utadhihirika zaidi kupitia miradi ya maendeleo iliyo chini ya Mpango wa Ukanda na Njia (Belt and Road Initiative) pamoja na Jukwaa la Ushirikiano wa Afrika na China (FOCAC), ambayo yamekuwa nguzo muhimu katika kukuza uchumi na miundombinu.
Kwa upande wake, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo aliishukuru Serikali ya China kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Tanzania, hususan kwenye utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya miundombinu, afya, elimu, nishati na viwanda. Alieleza kuwa Tanzania imedhamiria kuendelea kushirikiana na China katika kuvutia uwekezaji, biashara na teknolojia kwa lengo la kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Viongozi hao wawili walitumia fursa hiyo kujadili kwa kina masuala ya kihistoria yaliyoasisiwa na waasisi wa mataifa haya, wakisisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kindugu uliojengwa katika misingi ya kuheshimiana na kuaminiana. Aidha, waligusia masuala mbalimbali ya kisiasa na kijamii ambayo yamekuwa kiungo muhimu katika ushirikiano huo wa miongo mingi.
Mbali na masuala ya ndani, Mawaziri hao walijadili hali ya usalama na mshikamano katika ngazi ya kikanda na kimataifa. Walisisitiza haja ya kuimarisha mshikamano wa nchi zinazoendelea na kudumisha amani, huku wakihimiza kuwepo kwa mfumo wa kimataifa unaozingatia usawa na haki kwa mataifa yote.
Ziara hii ya Mhe. Wang Yi nchini Tanzania inaendelea kudhihirisha dhamira ya dhati ya nchi hizi mbili katika kuendeleza urafiki wao wa kudumu.
Mazungumzo hayo yamefanyika wakati ambapo ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na China umefikia viwango vya kihistoria:
Thamani ya Biashara:
Kwa mwaka 2024 pekee, thamani ya biashara kati ya nchi hizi mbili ilifikia takriban Dola za Marekani bilioni 5.2.
Miradi ya Uwekezaji:
Hadi kufikia mwaka 2025, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA) ilisajili miradi 343 ya China yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.1, ikizalisha jumla ya ajira 82,404 kwa Watanzania.
Sekta Muhimu:
Uwekezaji huo umelenga maeneo ya kipaumbele ikiwemo viwanda, kilimo, usafirishaji, mawasiliano, na utalii.
Urithi wa TAZARA na Miaka 60 ya Urafiki
Moja ya ajenda kuu katika ushirikiano huu ni uendelezaji wa miundombinu, ambapo reli ya TAZARA inasalia kuwa alama ya kudumu ya urafiki wa mataifa haya. Reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,860 ni kielelezo cha mshikamano ulioasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Mwenyekiti Mao Zedong.
Ziara ya Mhe. Wang Yi inathibitisha kuwa misingi ya kuaminiana na kuheshimiana iliyowekwa zaidi ya miongo sita iliyopita, inaendelea kuenziwa kwa vitendo na viongozi wa sasa, ikilenga kufungua fursa mpya za maendeleo kwa faida ya pande zote mbili.
Post a Comment