SAMIA AONYA WANAOCHOKOREWA MASIKIO KUVUNJA AMANI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa onyo kali kwa watu wanaojaribu kushawishi uvunjifu wa amani nchini, akisisitiza kuwa utulivu wa kisiasa ndio chachu kuu inayovutia wawekezaji wakubwa na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo mjini Unguja, Zanzibar, wakati wa hafla ya uzinduzi wa hoteli ya kitalii ya Jaz Elite Aurora, uwekezaji uliogharimu kiasi cha Dola za Marekani milioni 135 (takriban Shilingi bilioni 350 za Kitanzania).
Aidha, amesisitiza wananchi kulinda amani ya nchi, kwani maendeleo na kupendeza kwa nchi kunatokana na amani na usalama uliopo.
“Tusisahau kwamba kukua kwa uwekezaji nchini kunawezekana kutokana na uwepo wa amani, usalama na utulivu wa kisiasa. Sasa kwa wale wanaochokorewa masikio kuvunja amani ya nchi hii, niwasihi acheni mara moja kwani amani ikichafuka haichagui,” alieleza Rais Samia.
Alieleza kuwa tofauti za mawazo zipo lakini hazipaswi kuwagawa wala kuwafanya kuharibu utulivu na amani.
“Nilikuwa nazungumza na mwekezaji hapa, hoteli nyingine mbili atazifungua lakini akaninong’oneza kuna eneo kama ameshachukua, hajajenga lakini bado ameuliza maeneo mengine kama yapo. Huyu ni mmoja lakini wawekezaji wa aina hii wapo wengi, wanavutwa kwetu kwa usalama amani na utulivu wa nchi yetu,” alisema.
Rais Samia alisema sekta ya utalii nchini imeendelea kuimarika ambapo kuanzia mwaka 2022 hadi 2025, imeajiri zaidi ya Watanzania milioni 2.5 na idadi ya watalii wa nje na ndani iliongezeka hadi kufikia 5,360,247, ikilinganishwa na watalii 1,409,800 mwaka 2020.
“Kwa Zanzibar pekee, idadi ya watalii wanaokuja imeongezeka kutoka 743,606 mwaka 2024 hadi 816,000 mwaka jana na matarajio yetu na mambo haya yanayofunguliwa, idadi ya watalii itaendelea kuongezeka kuja kwetu Zanzibar,” alisema.
Aliongeza kuwa mchango wa sekta ya utalii kwenye pato la serikali kwa Zanzibar ni zaidi ya asilimia 30.
Alisema idadi ya hoteli zinazofanya kazi visiwani humo hadi kufikia mwaka jana imefikia 400.
“Niwapongeze Kampuni ya Reliance Resort and Tourism Limited kwa uwekezaji huu mkubwa wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 135, ni uwekezaji mkubwa haujapata kutokea Zanzibar. Hadi sasa, mradi wa ujenzi wa hoteli hii umefanikiwa kutoa ajira zaidi ya 158 kwa Watanzania wengi, wakiwa vijana wa Michamvi,” alifafanua.
Vilevile, Rais Samia alisisitiza kwamba katika uendeshaji, wahusika wahimize matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini na kwamba kazi ya wawekezaji ni kuwekeza na kuendesha shughuli za hoteli lakini shughuli zingine kama kuongoza watalii, zinapaswa kubaki kwa wenyeji.
“Niwahakikishie wawekezaji wote kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea kuweka mazingira rafiki na miundombinu wezeshi ili kuvutia wawekezaji wenye tija kama huyu,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Zanzibar, Sharif Ali Sharif alisema mafanikio makubwa yaliyopatikana Zanzibar ni pamoja na kuongezeka kwa miradi ya kimkakati ambayo imeongeza ushindani chanya, ubora wa huduma na hadhi ya Zanzibar katika soko la utalii la kimataifa.




Post a Comment