Vijana tukatae kugawanywa: Maandamano ni adui wa maisha ya mnyonge
Katika mwendelezo wa wito wa kudumisha amani na utulivu baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, na wakati kukiwa na wito wa baadhi ya wachochezi mtandaoni kuitisha maandamano mnamo Desemba 9, sauti za viongozi, wananchi wa kawaida, na Taasisi za kidini zinaendelea kusisitiza kuwa vijana wanapaswa kukataa kugawanywa na kutumiwa kwa maslahi ya wengine.
Wito huu unakuja wakati Umoja wa Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) ukitaka Serikali, viongozi wa dini, vijana na jamii kwa ujumla kuanza safari mpya ya maridhiano baada ya kadhia ya Oktoba 29 iliyoacha majeraha makubwa.
Sauti ya Mkulima:
Sirio Msimbe, mkazi wa Tchenzema Mgeta mkoani Morogoro na mkulima, ametoa ushuhuda wake akielezea jinsi vurugu za Oktoba 29 zilivyogusa moja kwa moja maisha ya Watanzania maskini.
"Maandamano ni adui wa taifa na adui wa maisha ya Watanzania maskini," alisema Sirio Msimbe kwa uchungu. "Vurugu zinasababisha mazao ya wakulima kama mimi, malimbichi, kukosa soko na kutengeneza hasara kubwa."
Msimbe alieleza kuwa wakati wa vurugu za Oktoba 29, zaidi ya tani mbili (2) za mazao yanayoharibika kwa haraka kama brokoli na maharagwe mabichi iliharibika kutokana na kukosekana kwa usafiri wa kwenda kwenye masoko. Alisisitiza kuwa wenye vyombo vya usafiri wanaposhindwa kusafirisha bidhaa kwa hofu ya vyombo vyao kuchomwa, kama ilivyokuwa Oktoba 29, wananchi wanakuwa kama wanakaanga maisha yao wenyewe.
"Vijana msikubali kuingia mtaani wala kufanya vurugu. Wengi wetu tunaingia kwa mkumbo tu kuwezesha maslahi binafsi ya watu," alihimiza Msimbe na kusema kufanya vurugu ni kuikasirisha dola na pia kuharibu mifumo ya maisha ambayo tayari inategemeana.
Wito wa JMAT:
Umoja wa Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) ulitoa tamko rasmi likielezea tukio la Oktoba 29, ambalo lilisababisha vifo, majeruhi, uharibifu wa mali za umma na binafsi pamoja na taharuki ya kitaifa, kama “jeraha la kitaifa linalohitaji uponyaji wa pamoja, hekima na majadiliano ya kina.”
Katika mkutano wa JMAT, Mchungaji Richard Hananja alitoa maneno ya hekima yaliyogusa wengi:“Changamoto zikitokea, hekima ni kumaliza changamoto bila kuzalisha changamoto nyingine. Maelewano yanapatikana kwa kiti na meza.”
Kauli hii inasisitiza ukweli kuwa njia ya mabadiliko ya dunia ya leo si mabavu, si hasira, si midomo yenye makali—ni mazungumzo, maridhiano, na kusikilizana kwa uaminifu.
Mchungaji Hananja aliongeza kuwa safari ya maisha, hususan safari ya mabadiliko, inahitaji jamii inayowezesha mazungumzo kuanzia ngazi za chini. Alishauri: “Hawa vijana wetu tukae nao kuanzia chini.”
Kuhusu changamoto ya ajira inayowakabili vijana wengi, Mchungaji Hananja alikumbusha ukweli wa msingi: "Elimu ndiyo uwekezaji mkubwa. Elimu ndiyo mbolea ya akili... Ukiwa na Elimu hushindwi.”

Post a Comment