TUSIRUDI NYUMA TENA: Kulinda Amani Ndio Msingi wa Dira ya Taifa ya 2050
Picha za CCTV na kumbukumbu za vurugu zilizotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, zimebakia kuwa somo chungu na wito wa dhati kwa Taifa: Vitendo vya uharibifu na uchochezi havipaswi kujitokeza tena. Serikali, wadau wa maendeleo, na vijana wenyewe wanasisitiza kwamba uharibifu wa mali na ukiukwaji wa utu hauna nafasi katika Tanzania inayoendea uchumi wa kati wa juu.
Katika kila kumbukumbu ya tukio la kutisha la Oktoba 29 wito unatolewa na vijana wenyewe wakisisitiza kwamba jukumu la kulinda amani linaanzia kwao, kwa kutambua kuwa maendeleo hayawezi kustawi kama kuna moto wa chuki na mgawanyiko.
“Amani si tu ukosefu wa vita, bali ni hali ya utulivu, heshima, na umoja inayotuwezesha kujenga pamoja.” – Kauli ya Vijana Wanaopenda Amani.
Ujumbe huu unasisitiza misingi mikuu ya kuepuka kurudia makosa ya zamani kwa kila Mtanzania ni Balozi wa Amani.
Wengi wamekiri kuwa umaskini hauwezi kuisha kwa siku moja, lakini amani inaweza kuisha kwa siku moja na kuleta tabu kubwa kuirudisha. Vijana wanahimizwa kutokubali 'njaa na matumbo' viwaongoze kufanya ujinga wa aina hii.
Dira ya Taifa ya Tanzania 2050 imeweka wazi maono ya nchi yetu kuwa kitovu cha viwanda katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini. Lengo hili la kufikia Uchumi wa Kati Ngazi ya Juu, wenye pato la mtu mmoja la Dola za Marekani $7,000 kwa mwaka, linatekelezeka tu chini ya mazingira ya amani na utulivu.
Maono haya makubwa yanakinzana moja kwa moja na vitendo vya kihujuma kama vile kuharibu miundombinu iliyojengwa kwa kodi za walipa kodi, kuiba mali za wananchi, na kuvuruga maisha ya watu wasio na hatia. Vitendo kama hivyo vinaelezwa kuwa ni uhujumu wa uhuru wetu na kujaribu kuirudisha nyuma Tanzania iliyojengwa kwa miaka mingi.

Post a Comment