NEEMA YA BILIONI 50 KUFUNGUA UKURASA MPYA KWA WATENGENEZA MAUDHUI




Ni shangwe na vifijo kwa vijana wanaojihusisha na sekta ya ubunifu, sanaa, na habari nchini baada ya Serikali ya Awamu ya Sita kufungua rasmi milango ya utajiri kupitia mfuko wa Shilingi Bilioni 50.

Hatua hii si tu ushindi kwa watengeneza maudhui (content creators) bali ni matokeo ya dhati ya maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameamua kuweka fedha mkononi mwa vijana ili kukuza uchumi wao kupitia vipaji. 

Akizungumza jijini Arusha Machi 11, 2026, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, amethibitisha kuwa kilichokuwa kilio cha muda mrefu cha mitaji kwa wabunifu sasa kimepata mwarobaini wa kudumu.

Ushindi huu umekuwa mkubwa zaidi baada ya Wizara kufanya mazungumzo ya kimkakati na Benki ya CRDB, ambapo kiwango cha fedha kimeongezeka maradufu kutoka Bilioni 20 zilizopangwa awali hadi kufikia Bilioni 50. Ongezeko hili ni kielelezo cha imani kubwa ambayo taasisi za kifedha na serikali wanayo kwa vijana wa Kitanzania, likiwa ni lengo la kupanua wigo ili kila kijana mwenye wazo la kiubunifu, mwandishi wa habari, influencer, na msanii aweze kunufaika. 

Matokeo haya yanakwenda kubadilisha sura ya tasnia ya habari na sanaa nchini, ikihama kutoka kwenye kufanya kazi kwa mazoea na kuelekea kwenye biashara yenye tija na faida kubwa.

Kilele cha shangwe hizi kinatarajiwa hivi karibuni ambapo mgeni rasmi, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi mfuko huo na kuanza kugawa neema hiyo kwa walengwa. 

Vijana sasa hawatakuwa tu wasikilizaji wa sera, bali washiriki wa moja kwa moja wa uchumi wa taifa kupitia kazi za mikono na bongo zao. 

Hii ni tano nyingine kwa serikali ambayo imetambua kuwa nguvu ya vijana katika mitandao na sanaa ni fursa ya kiuchumi, ikigeuza vipaji vyao kuwa chachu ya maendeleo ya Tanzania ya kisasa.

No comments