Rais Samia atoa msamaha kwa wafungwa 1,036 Kuadhimisha Miaka 64 ya Uhuru
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa msamaha kwa jumla ya
wafungwa 1,036 katika kuadhimisha Miaka 64 ya Uhuru wa Tanzania Bara leo
Disemba 9, 2025.
Msamaha huo umetolewa
na Mheshimiwa Rais kwa kutumia Mamlaka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(a)-(d)
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.
Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, George B. Simbachawene , alitoa taarifa hiyo kwa umma leo kutoka
Dodoma, Makao Makuu ya nchi.
Kati ya wafungwa 1,036 walionufaika na msamaha huo,wafungwa 22 wameachiliwa huru leo tarehe 09 Disemba, 2025 na 1,014 wamepunguziwa adhabu zao na
watabaki gerezani na kuendelea kutumikia sehemu ya vifungo vilivyobaki.
Serikali imeeleza
kuwa inatarajia wafungwa walioachiliwa huru watarejea tena katika jamii
kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa Taifa na watajiepusha kutenda
makosa ili wasirejee tena gerezani11.
Msamaha
huo ambapo wafungwa wote wenye sifa stahiki wanapunguziwa moja ya sita ya
adhabu zao wanazozitumikia, baada ya punguzo la kawaida la moja ya tatu umewakuta wafungwa waliokaa kifungoni kuanzia miaka miwili na kuendelea na
wametumikia robo ya adhabu zao gerezani, na wameingia gerezani kabla ya tarehe
15 Oktoba, 2025.
Pia kuna makundi maalumu kama wafungwa
wagonjwa wenye magonjwa ya kudumu au sugu walio kwenye hatua ya mwisho,
wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini (70) au zaidi , wafungwa wa kike
walioingia na ujauzito au wenye watoto wanaonyonya au wasionyonya , na wafungwa
wenye ulemavu wa mwili na akili wasio na uwezo wa kufanya kazi. Uthibitisho wa
umri, ugonjwa, au ulemavu unatakiwa kufanywa na jopo la waganga chini ya Mganga
Mkuu wa Mkoa/Wilaya.
Aidha Waziri
Simbachawene alifafanua kuwa msamaha huo hauwahusishi wafungwa waliofanya makosa mazito, ikiwemo:
- Makosa ya Kiuchumi na Rushwa: Uhujumu uchumi, matumizi mabaya
ya madaraka, utakatishaji wa fedha, rushwa na usafirishaji wa madawa ya
kulevya.
- Ukatili dhidi ya Binadamu: Makosa ya kujamiana, utekaji au
wizi wa watoto, kuwapa mimba wanafunzi, na biashara haramu ya binadamu.
- Makosa ya Kijambazi: Unyang'anyi, unyang'anyi wa
kutumia nguvu, unyang'anyi wa kutumia silaha.
- Makosa Mengine: Wizi au ubadhirifu wa fedha za serikali
, makosa ya kujihusisha na nyara za Serikali au ujangili , ugaidi na
uharamia, makosa ya mauaji , na wafungwa wanaotumikia kifungo cha maisha.

Post a Comment