Piga namba hizi kusaidia kunasa wachochezi wa mtandaoni, Hali ya usalama shwari
Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetoa wito kwa wananchi wanaowafahamu watu wanaoshiriki katika makundi ya mtandaoni yanayoeneza taarifa za uzushi, uchochezi, na uongo zenye lengo la kuhamasisha vurugu na vitendo ambavyo ni kinyume na sheria, watoe taarifa haraka iwezekanavyo kwao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Makao Makuu ya Polisi, Dodoma, Makosa ya Kimtandaoni (Cybercrimes) na yale yanayohusisha uvunjifu wa sheria hayatasamehewa. Jeshi hilo limetoa namba za simu za kutoa taarifa kwa siri, ambazo ni: 0699 99 88 99, 0787 66 83 06, au kupitia kiunganishi cha mtandaoni: https://taarifa.tpf.go.tz.
Wito huu umetolewa huku Jeshi la Polisi likijulisha umma kwamba, hadi jioni ya leo tarehe 10/12/2025, hali ya nchi kiasalama, hasa katika shughuli za kiuchumi na kijamii, inaendelea katika mazingira ya amani na utulivu.
Taarifa ya Polisi inasisitiza kwamba wito huo umelenga kuhakikisha usalama unadumishwa kwa kupata taarifa za mapema kuhusu watu wanaojaribu kuharibu amani hiyo kupitia mitandao. Wananchi wameombwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha utulivu na amani ya nchi inalindwa kwa manufaa ya wote.

Post a Comment