Mbunge Jenista Mhagama Aaga Dunia, Rais na Spika Waomboleza, Peramiho waona giza
Taifa la Tanzania limegubikwa na huzuni na majonzi mazito kufuatia kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Peramiho, kilichotokea leo Mkoani Dodoma.
Marehemu Mhagama alikuwa kiongozi mahiri, mnyenyekevu, na mchapakazi aliyejitolea kulitumikia Taifa katika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Serikali na Bungeni.
Taarifa za msiba huu zilitolewa rasmi na Ofisi ya Bunge pamoja na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, zikithibitisha kuondokewa na kiongozi huyo ambaye alikuwa Mwakilishi wa Wananchi wa Jimbo la Peramiho.
Salamu za Rambirambi Kutoka Ikulu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kwa Spika wa Bunge, Mheshimiwa Musa Azzan Zungu, na Taifa zima.
Katika salamu zake, Rais Samia amemuelezea marehemu Jenista Mhagama kama kiongozi makini na mchapakazi aliyekuwa na mwenye historia ndefu ya kulitumikia Taifa kwa uadilifu.
“Ninatoa pole kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Musa Azzan Zungu, wananchi wa Jimbo la Peramiho, familia, ndugu, jamaa na marafiki, na kuwaombea wote Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu,” amesema Rais Dkt. Samia.
Bunge Laomboleza Kifo cha Ghafla
Kupitia taarifa iliyotolewa na Spika wa Bunge, Mheshimiwa Musa Azzan Zungu, alisema ofisi hiyo imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mbunge huyo.
"Kwa masikitiko makubwa, naomba kutangaza kifo cha Mbunge wa Peramiho Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama kilichotokea leo 11 Desemba, 2025 Jijini Dodoma. Natoa pole kwa Waheshimiwa Wabunge wote, familia ya Marehemu, ndugu, jamaa na Wananchi wa Jimbo la Peramiho. Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu,” alieleza Spika Zungu.
Ofisi ya Bunge imeongeza kuwa itaendelea kutoa taarifa zaidi za mipango ya mazishi. Kwa sasa, viongozi na wananchi wanaendelea kutoa pole na maombi kwa familia ya Marehemu.
Peramiho
Nyumbani Perahamiho wananchi wenye simanzi wamekusanyika wakimuelezea kwamba alikuwa karibu sana na watu na pia alikuwa mchangiaji hodari wa huduma za jamii hasa kusaidia wasiojiweza na wenye mahitaji maalumu.
Kauli hiyo imetolewa na Mwalimu Juma Nyumayo na pia mwandishi wa habari Crasencxe Kapinga alielzea jinsi alivyomsaidia katika kumwelekeza maisha.
Mhagama, aliyezaliwa Juni 23, 1967, alikuwa Mbunge kwa miaka kadhaa, alimrithi Ummy Mwalimu kama Waziri wa Afya, ambaye utumishi wake katika nafasi hiyo ulidumu kwa miaka 14.
Mnamo Desemba 2015, aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, anayehusika na Sera, Masuala ya Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu katika utawala wa Rais John Magufuli.
Mnamo Januari 2022, alihamishiwa Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora.
Mhagama alianza kujihusisha na CCM kwa mara ya kwanza mwaka 1987 na aliwahi kuhudumu katika majukumu mbalimbali, ikiwemo katika jumuiya za vijana na wanawake za chama hicho. Aliteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mbunge kupitia viti maalum vya wanawake mwaka 2000.
Mwenyezi Mungu ailaze Roho ya Marehemu Jenista Joakim Mhagama mahali pema Peponi, Amina.

Post a Comment