Makamu wa Rais Dkt. Nchimbi Aomboleza Kifo cha Jenista Mhagama; Atajwa Kuwa Kiongozi Aliyeheshimika

 



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ameeleza kuwa Taifa limepata pengo kubwa kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma, marehemu Mhe. Jenista Joakim Mhagama (1967-2025).

Akitoa salamu za rambirambi nyumbani kwa marehemu eneo la Itega, Jijini Dodoma, Makamu wa Rais alimwelezea Marehemu Mhagama kama kiongozi aliyeheshimika na kutumikia nchi kwa uaminifu katika majukumu mbalimbali ya kitaifa. Dkt. Nchimbi alisisitiza kuwa mbali na kuwa Mbunge wa Peramiho, marehemu pia alitoa mchango mkubwa katika Chama Cha Mapinduzi na kusimamia maendeleo ya Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.

"Marehemu Mhagama alikuwa kiongozi aliyeheshimika na kutumikia nchi katika majukumu mbalimbali ya kitaifa," alisema Makamu wa Rais, akisisitiza umuhimu wa kiongozi huyo katika maisha ya kisiasa na maendeleo ya jamii.



Makamu wa Rais alitoa pole kwa familia na waombolezaji, akiwaombea watoto wa marehemu na ndugu wa karibu Mungu awape ujasiri wa kukubali jambo hilo, akitambua kuwa huo ni mwisho wa kila mwanadamu.

Ratiba ya Mazishi Kuendelea kwa Siku Nne

Kulingana na ratiba iliyotolewa na Bunge la Tanzania, mwili wa Marehemu Mhagama ulitarajiwa kuwasili nyumbani Dodoma (Itega) mnamo Desemba 12, 2025 saa 11:00 Jioni kwa ajili ya maombolezo.

Ratiba ya mazishi, ambayo inaendelea hadi Desemba 16, 20257, inajumuisha hatua zifuatazo:

Tarehe

Tukio Muhimu

Mahali

Desemba 13, 2025 (Jumamosi)

Ibada, Salamu za Rambirambi na Heshima za Mwisho

Kanisa Katoliki, Kiwanja cha Ndege, Dodoma.

Safari ya kuelekea Songea Alasiri.

Desemba 14, 2025 (Jumapili)

Ibada na Maombolezo.

Nyumbani kwa Marehemu Makambi, Songea Mjini na Kanisa Katoliki Matogoro.

Desemba 15, 2025 (Jumatatu)

Ibada na Salamu za Rambirambi.

Kanisa la Katoliki Peramiho, Songea Vijijini.

Wananchi wa Peramiho kuaga mwili.

Kanisa la St. Joseph Peramiho, Songea Vijijini.

Desemba 16, 2025 (Jumanne)

Mazishi.

Kijiji cha Ruanda, Wilayani Mbinga.



Makamu wa Rais Dkt. Emmanuel Nchimbi anatarajiwa kuwa miongoni mwa viongozi wakuu watakaotoa salamu za rambirambi wakati wa ibada za kumwaga marehemu Dodoma na Peramiho.

 

No comments