TIMU ya Taifa ya Tanzania ya soka la ufukweni (Beach Soccer)
inatarajiwa kucheza na timu ya Taifa ya Misri
Machi 13 mwaka huu kwenye ufukwe wa Escape one Msasani jijini Dar es
Salaam.
Mchezo huo wa raundi ya pili wa kutafuta kufuzu fainali za Afrika
zitakazo fanyika visiwa vya Shelisheli utaanza majira saa 10 kamili jioni.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Afisa habari wa
Shirikisho la Soka nchini (TFF), Baraka Kizuguto, alisema kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania
kinaendelea na mazoezi kujiandaa ya mchezo huo, ambapo kwa takribani wiki mbili
kipo kambini Bamba Beach wakijifua.
“Timu yetu ipo Kambini Bamba Beach ikiendelea na mazoezi kwa ajili
ya mchezo na Misri kwani ni mchezo muhimu kushinda ili kufuzu kwa fainali za
Afrika”, alisema Kizuguto
Tanzania ilifuzu hatua ya pili baada ya kuiondoa timu ya Taifa ya
Kenya kwa jumla ya mabao 12 -9, na endapo itafanikiwa kuwaota Misri, itafuzu
moja kwa moja kucheza Fainali za soka la Ufukweni zitakazofanyika Visiwa vya
Shelisheli mwezi April mwaka huu.
Pia alisema aamuzi wa mchezo huo ni Eid Haitham Eid Hassan toka
Sudan, mwamuzi msaidzi namba moja ni Abaker Mohamed Bilal wa Sudan pia.
Mwamuzi msaidizi namba mbili ni Abdalla Hassain Hassaballa, mtunza
muda ni Boubaker Bessem wanatoka Tunisia, wakati kamisaa wa mchezo huo ni Khiba
Herbert Mohoanyane kutoka Lesotho.
Mchezo wa marudiano unatarajiwa kufanyika wiki ijayo nchini Misri
kati ya Machi 20,21 na 22 mwaka huu.
Timu ya Taifa ya Misri inatarajiwa kuwasili Dar es salaam leo mchana,na itafikia katika hoteli ya Double Tree by
Hilton iliyopo Masaki pia waamuzi wanatarajiwa kuwasili leo na watafikia katika
hotel ya Protea Oysterbay.
Pia kesho makocha wa timu zote wataongea na vyombo vya habari
katika ukumbi wa mikutano wa TFF uliopo Karume kuanzia majira ya saa 5 kamili
asubuhi.
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), inaitakia
kila la kheri na ushindi timu ya Taifa ya soka la ufukweni (Beach Soccer)
katika huo dhidi ya Misri.
No comments:
Post a Comment