Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Tuesday, March 10, 2015

SIMBA SC ILIWAMALIZA YANGA SC NA 4-4-2 FLAT YAO"

Ikitumia mifumo ya 4-1-2-3 ambao ulikuwa ukibadilika na kuwa 4-3-3 wakati wa kushambulia na kukaba timu ya soka ya Simba SC iliipoteza kabisa timu Yanga SC katika eneo la katikati mwa Uwanja ambapo walionekana vijana wawili mahiri Saidi Hamisi Ndemla na Jonas Gerard Mkude wakipatawala vizuri mno huku Abdi Hassan Banda akiwalinda mabeki wake wa kati Juuko Mursheed na Hassan Isihaka katika aina ile ile iliyompatia umaarufu mkubwa mchezaji Claude Makelele raia wa Ufaransa katika ile inayoitwa “Makelele Role”.

Yanga SC iliyocheza katika mfumo wa 4-4-2 katika muda mwingi wa mchezo huo ilijikuta ikizidiwa sehemu ya kati ya uwanja ambapo waliwachezesha viungo asilia wawili tu huku wakimtumia Mrisho Ngassa kama namba 10 na Msuva na Mrwanda kama viungo wa pembeni, hivyo kufanya eneo la kati la uwanja litawaliwe na Simba ambao walichezesha viungo Asilia wa kati wanne ambao ni Ndemla aliyetumika upande wa kushoto juu kidogo ya Mohamed Hussein “Tshabalala”, Mkude kati juu kidogo ya Abdi Banda na Ibrahim Ajib nyuma ya Emmanuel Okwi.

 Kocha mkuu wa Simba Goran Kopunovic kwa kuisoma nguvu ya wapinzani wake akaamua kuanza na timu ambayo haikuwa na Mshambuliaji wa kati asilia hivyo kuongeza namba ya kiungo Mmoja ambae kwa siku za karibuni ametokea kuwa ni Abdi Banda ambae amekuwa akimtumia kuwalinda mabeki wake wa kati huku akiihimiza timu yake iwabane wapinzani kwa kuwakaba kwa karibu kwa idadi ya namba kubwa ya wachezaji inaitwa “Pressing football” muda wote wanapokuwa na mpira wapinzani na kuwataka kucheza pasi nyingi muda wote wanapokuwa wanamiliki mpira wao.

Hans van Pluijm kocha mkuu wa Yanga alitumia Mfumo wake wa 4-4-2 huku akihimiza 
washambuliaji wake wa pembeni ambao walikuwa wanaongozwa na Msuva na Mrwanda kupeleka mashambulizi mazito kwa Simba, mbinu ambayo haikuweza kufanikiwa kutokana na aina ya mpira waliokuwa wanacheza Simba kuwa na Wachezaji wengi katika kila Idara, 4-1-2-3 iliwawezesha Simba kuwa na Mabeki watano waliposhambuliwa na kuwa na washambuliaji watatu na Viungo wawili waliposhambulia.

Saidi Hamisi Ndemla alitumika kumpa ulinzi Mohamed Hussein Tshabalala upande wa kushoto wa Simba na kumfanya Msuva kuwa na nafasi finyu ya kukimbia alikadharika Ramadhan Singano alitumika muda wote kumsapoti Hassan kessy upande wa kulia hivyo kumfanya Mrwanda kushindwa kutengeneza mipango ya kushambulizi ya Yanga huku Mkude akitumika kuiunganisha Timu kutoka kwa Abdi Banda na mabeki kwenda kwa Ibrahim Ajib na Okwi.

 Saidi Juma Makapu kiungo wa Ulinzi wa Yanga alifanya kazi yake ipasavyo muda wote anastahili pongezi lakini kukosa muunganiko kati yake na Niyonzima ilikuwa pigo kwa Yanga, kuna muda Niyonzima alionekana akicheza nyuma ya Juma, kuna kipindi Niyo alionekana kucheza Pembeni ya Juma na kadhalika mbele ya Juma, kosa kubwa Juma hakuwa na “Movement” za kutoka pale alipocheza kwenda mbele lakini aliweza kupiga “tackle” za akili na kutoa mipira nje au kutoa pasi kwa wenzie alichozidiwa ni pale alipokuwa anakabiliana na Ndemla, Mkude na Ajib kwa wakati Mmoja alishindwa kujua afanye nini, ilipelekea kupewa kadi ya njano baada ya kupitwa na Ajib na kumvuta jezi baada ya pasi za mguso za Simba SC.

Mabeki wa pembeni wa Yanga SC Mbuyi Twite na Oscar Joshua pamoja na kutokuwekwa bize na viungo wa pembeni wa Simba SC kwa muda wote wa mchezo hawakuwa mchezoni kwa kupandisha mashambulizi walicheza kwa uoga na kwa kuwa Simba walikuwa wanacheza zaidi katikati mwa uwanja muda wote wa mchezo waliwafanya mabeki hawa wawe abiria muda wote wa Mchezo hata goli la Okwi Mbuyi Twite hakuwa “aggressive enough” kuziba njia ya Okwi aidha asipige au Asimpite badala yake alisimama mbele ya Okwi kumfanya asiucheze mpira kwa haraka labda kwa kupiga krosi au kuendelea kuwa nao miguuni.

Upande wa Simba Hassan Kessy aliweza kupanda mbele katika muda mchache wa mechi katika kipindi cha kwanza na kusababisha faulo mbele ya lango la Yanga lakini haikuzaa matunda, Mohamed Hussein alikua anaishia katikati mwa Uwanja muda wote alibaki kwenye mbinu halisi za mwalimu wake, Juuko Mursheed na Hassan Isihaka hawakuwa na wakati mgumu kwa vipindi vyote viwili maana kazi zilimalizwa na Banda na wao alicheza kwa akili muda wote mipira iliyodondoka miguuni mwao, na mipira yote ya Juu Juuko aliweza kuidhibiti kutokana na Kimo chake, Mabeki hawa wakati walikuwa ndio waanzilishi wa mipira yote ya Simba SC hawakubutua hovyo mipira ila pale tu ilpobidi kwa kuokoa hatari.

 Ibrahim Ajib alicheza namba 10 upande wa Simba alikuwa anatuliza mpira anatoa pasi ama kuendesha kwenda mbele na kwa kuwa Simba walikuwa na faida ya namba ya wachezaji upande wa kushambulia na kukaba (Numerical Advantage) hivyo Ajib hakuwa akizongwa na watu wengi, hata pasi aliyompa Okwi na kuzaa goli inathibitisha hilo alipokea mpira uliookolewa baada ya kupigwa kona kwenye lango lao, akageuka na mpira akavuta mara moja na kutoa pasi maridhawa kwa Okwi na yeye kuanza kukimbia kwenye goli la Yanga na kusababisha wachezaji wawili wa Yanga kuanza kukimbia nae.

Emmanuel Okwi huyu ndio aliamua mechi kwa kupeleka ushindi Simba SC, goli lake ni miongoni mwa Magoli bora kupata kufungwa kwenye Nyasi za uwanja wa Taifa, hakika goli lile litabaki kwenye kumbukumbu za washabiki na wafuataliaji wa mambo ya Soka kwa muda mwingi sana hasa hasa kulifunga katika mechi ya Watani wa Jadi na kuipa ushindi Timu yake ya Simba SC.

 Upande wa Yanga Msuva, Ngassa na Tambwe hawakuweza kuipenya ngome ya Simba kutokana na Faida ya Namba ya wachezaji waliyokuwa nayo Simba Sc katika mechi ya jana, ilitokea mara moja tu Yanga waliweza kuipenya ngome ya Simba katika Kipindi cha kwanza ambapo shambulizi lao kali lilishia kuwa goal kick baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Simba SC.

 Mabadiliko ya kuingia Hussein Javu na Kpah Sherman kwa Yanga hayakuwasaidia sana, japo Javu aliweza kupiga mpira mmoja langoni mwa Simba uliookolewa na Kipa Ivo Mapunda na kuwa kona mfu, nafikiri kocha wa Yanga alipomtoa Danny Mrwanda alipaswa kumuingiza Salum Telela na kubadili mfumo kutoka 4-4-2 na kwenda 4-2-1-3 kwa kumfanya Makapu kucheza na Telela huku Niyonzima akiwa free role pale kati juu ya viungo wawili na Ngassa kwenda kucheza upande wa Kushoto na kumuacha Tambwe kati peke yake huku Msuva akibaki upande ule ule wa kulia, naamini mabadiriko haya yangeweza kuwasaidia kupambana katikati ya uwanja baada ya mbinu ya kupitia pembeni kushindwa kufanya kazi.  

KASORO NILIZOZIONA

  1. Mpira ulichezwa dakika 70 na sio 90 kama sheria inavyotaka Mechi za Simba na Yanga siku za hivi karibuni zimekuwa zikichezwa kwa dakika 70 tu na si zaidi ya hapo, Makocha na Wachezaji wamekuwa wakitumia mbinu nyingi sana kuufanya mpira uwe umepoa na usiokuwa na papara kitu kizuri, lakini vitendo vingi vinavyotokea Uwanjani baina ya wachezaji kwa makusudi kabisa vinapelekea muda wa mpira kuchezwa kutotimia, kwa siku ya jana kulikuwa na kusukumana na kusimama mpira kwa mara kadhaa, yafuatayo ni baadhi ya matukio yaliyokula muda;
kuumia kwa Ally Mustapha “Barthez” alipogusana na Ramadhan Singano alitumia dakika 2 pale chini. Kusukumana kwa Danny Mrwanda na Hassan Kessy kulitumia dakika moja na nusu kufikia muafaka, kuumia kwa Ivo baada ya lango lake kupewa misukosuko alitumia dakika 2, na muda huo wakati madaktari wanaondoka walilirudisha taulo ambalo awali lilitolewa hivyo kumfanya Refa kurudi tena pale golini kumwambia Ivo alitoe sekunde thelathini, Kuumia kwa Nadir Haroub na kupewa tiba uwanjani kwa takribani dakika tatu wachezaji wa yanga wakalalamika atolewe nje akatibiwe kwanza wakiongozwa na Mrisho Ngassa na Kelvin Yondani, Kuumia kwa Okwi kulitumia dakika moja hadi anatolewa nje lakini alipofika nje tu akashikwa shikwa Enka yake na kurudi uwanjani. Kufanya mabadiriko kwa wachezaji wa Timu zote mbili Simba Ajib na Banda kuwapisha Maguri na Simon Sserunkuma walitumia dakika mbili kwa pamoja, Yanga kwa upande wao walitoka Mrwanda mapema na Ngassa na kuingia Hussein Javu na Kpah Sherman wao muda ulitumika kama dakika moja kwa wote kutokana na Matokeo kuwa dhidi yao. Kadi nyekundu ya Niyonzima baada ya kadi ya njano ya pili, mpira ulisimama kwa takribani dakika nne hapa unaweza kusema ni kwa Uzembe wa mchezaji wa timu iliyopewa kadi kubisha kutoka nje, kwa tukio kama hili Refa hawezi kusimamisha saa yake. Ukikusanya muda wote uliopotea kwa mpira kusimama kwa matukio hayo, ukijumlisha na mipira iliyotoka kuwa ya kurusha, kupigwa (goal kick) na kona ukija kuangalia na dakika zilizoongezwa kufidia muda utaona ni jinsi gani mpira ulichezwa kwa dakika sabini tu!

2. Waamuzi wetu Mwamuzi Martin Saanya ni kama alikuwa anaogopa Siasa za Timu hizi mbili yeye na washika vibendera wake, mimi niliyekuwa nimekaa Jukwaani niliona tukio la Danny Mrwanda kumshambulia kwa kumvamia Hassan Kessy na alistahili kupewa kadi Nyekundu lakini si kwa Saanya na Wasaidizi wake. Juuko Mursheed na Kelvin Yondani huwa kuna muda sielewi kwanini wachezaji huwa wanafanya matukio ya kijinga uwanjani hasa pale mpira unapokuwa umesimama, lilitokea tukio la kusukumana wakati kona anaenda kupigwa katika lango la Yanga, na kutokea kusukumana kwa wachezaji hao wawili baada ya sintofahamu ile Juuko alionekana kabisa kumpiga kiwiko Kelvin ambae muda wote alikuwa anamsukuma na kumfanyia vitendo visivyo vya kimchezo Juuko, Mimi nikiwa jukwaani niliona tukio lile lakini kwa mshangao wa wengi alipoulizwa Mshika kibendera alitoa ushauri ambao Bwana Saanya aliishia kutoa kadi za njano kwa wachezaji wale wawili.  Nadir Haroub Ally na faulo zake mbili kwa Ibrahim Ajib na Emmanuel Okwi, ikifika siku waamuzi wakachezesha kwa kufuata Sheria zote 17 za mpira naamini wachezaji wengi wa timu hizi hawatamaliza mechi.

  3. Taulo la Ivo Hii ni Ajabu na Aibu kwa soka letu, Chama cha Waamuzi (FRAT), Chama cha Soka Tanzania (TFF), na Asasi zote zinazojishughulisha na Mpira wetu, Mpira unaonyeshwa Dunia nzima hivi tunataka kuwaambia nini watu wa Dunia nyingine kuhusu Taulo kukaa langoni?, Tumeona makipa wengi Ulimwenguni kote Kama Peter Schemeicher aliyekuwa Manchester United, David Seaman Arsena FC, Jens Lehmann Arsena FC na wa Kizazi cha sasa kama Manuel Neuer wa Bayern Munich, Joe Hart wa Manchester City wakiambatana na Mataulo yao Golini, Lakini hili Taulo la Ivo Mapunda linachukua sura ya kipekee sana hadi Mwamuzi kushinikiza litolewe sasa sijaelewa Tatizo la lile Taulo ni nini? Kama Taulo lile lilikuwa lina uwezo wa kuzuia Magoli mbona lilipoondolewa Yanga Hawakufunga hilo Goli? Ni muda muafaka sasa kubadilisha hisia zetu, mawazo yetu na akili zetu zifikirie juu ya mambo makubwa sio haya ya mizaha mizaha tu kila siku, sitaki kuamini yule Mwamuzi kwanini aliingia kwenye ule Mtego? Sio yeye tu waamuzi wengi wamekuwa wakiingia kwenye mitego ya kipuuzi kama ile, na kutokana kuwa na waamuzi wasiojiamini Mechi za Simba na Yanga zinachezwa muda mchache mno na Dakika nyingine nyingi zinapotezwa kwenye mambo kama haya. Inasikitisha taulo la Ivo kuonekana sana kuliko viwango vya wachezaji wetu. 
 Kwa msaada wa mtandao wa http://www.simbamakini.com

No comments:

Post a Comment