Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Sunday, August 11, 2013

SUAREZ ATAIPIKU BEI YA NYOTA HAWA


LONDON, England
HARAKATI za Arsenal kumshawishi Luis Suarez juzi zilichukua sura mpya, baada ya kocha wa timu hiyo, Arsene Wenger, kuweka wazi kuwa anataka  kuvunja rekodi ya usajili ndani ya timu hiyo ya  Gunners, ili kuhakikisha anamnasa nyota huyo wa Liverpool.

Mbali na kuvunja rekodi ya usajili ndani ya klabu yake, kocha wa klabu hiyo ya Emirates, alitangaza kuvunja rekodi ya usajili nchini humo kwa kupanda hadi kufikia dau la pauni milioni 51, ili kuhakikisha anatimiza azma  yake.

Hadi sasa rekodi ya usajili ndani ya Arsenal  ni pauni milioni 15, ambazo ilizitoa kumsajili, Andrey Arshavin mwaka 2009, lakini kwa sasa Arsenal inaripotiwa kudhamiria kuondokana na rekodi hiyo kwa kumnyakua Suarez.

Hadi sasa Arsenal imeshapeleka ofa karibia mara tatu ikiomba kumsajili mshambuliaji huyo raia wa  Uruguay, lakini inavyoonekana Liverpool haijaonesha dhamira yoyote  ya kupokea ofa hizo kutoka kwenye klabu hiyo ya Kaskazini mwa jiji la London.

Inaelezwa  kuwa Arsenal, safari hii imedhamiria kuweka mezani dau la pauni milioni 51 kumchukua  Suarez  kutoka  Liverpool, kiasi ambacho kitakuwa kimezidi cha pauni milioni 50 ambazo klabu hiyo ililipwa na Chelsea wakati ikimsajili Fernando Torres  mwaka  2011.
Endapo Arsenal itaipiku rekodi ya Torres, itakuwa imemfanya Suarez kuwapiku nyota wengine kumi ambao walisajiliwa  kwa bei mbaya miaka ya nyuma.
Ifuatayo ni orodha ya wachezaji hao ambao wamewahi kutikisa rekodi ya usajili nchini England, ambao kama dili la Suarez litafanikiwa atakuwa amewabwaga.


10. Andriy Shevchenko: AC Milan kwenda Chelsea: pauni milioni 30.

Kuwasili kwa, Andriy Shevchenko  kwenye klabu hiyo ya  Stamford Bridge kulifanikishwa mno na mmiliki wa timu hiyo, Roman Abramovich kuliko aliyekuwa  kocha wa timu hiyo na ambaye amerejea kwa mara ya pili, Jose Mourinho.
Abramovich inadaiwa  ndiye aliyewabembeleza mno mashabiki wa  AC Milan hadi akafanikiwa kumnasa.

Hata hivyo Shevchenko, hakuweza kufunga mabao kama alivyofanya akiwa  kwenye klabu hiyo ya  San Siro na nyota huyo anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji walionunuliwa kwa bei mbaya  na Abramovich, lakini wakashindwa kuleta manufaa kwa Chelsea.
Katika kipindi alichokipiga kwenye klabu hiyo mchezaji huyo wa timu ya Taifa  Ukraini alijikuta akiziona nyavu mara  22 katika mechi  77 alizoshuka uwanjani kuchezea Chelsea, kabla ya  kumwaga mbio kwenye  Klabu hiyo ya Magharibi mwa jiji London na kwenda kukipiga  Dynamo Kyiv, ikiwa ni baada ya kuitumikia miaka mitatu tu.


9. Rio Ferdinand: Leeds  kwenda  Manchester United kwa pauni milioni 30

Ferdinand

Rio Ferdinand aliingia kwenye historia ya wachezaji waliosajiliwa kwa bei mbaya katika usajili wa Uingereza alipojiunga na Manchester United akitokea  Leeds  wakati wa usajili wa majira ya joto ya mwaka  2002.

Hata hivyo, beki huyo wakati huo  alishaweka rekodi nyingine alipotoka  West Ham kwenda Leeds miaka miwili kabla ya kujionesha mwenyewe kuwa ni kinda bora kwenye klabu hiyo ya  Upton Park.

Ferdinand alishashuka uwanjani mara  430 katika kipindi cha miaka  11 alichoitumikia  Manchester United  akiwa kama mchezaji na kuisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara sita na ubingwa mara moja wa michuano ya Klabu Bingwa Ulaya.

8. Dimitar Berbatov: Tottenham kwenda  Manchester United –kwa pauni milioni 30.8


Rio Ferdinand alipoteza nafasi yake ya kuwa mchezaji aliyesajiliwa kwa bei mbaya kwenye klabu hiyo ya  Manchester United wakati ilipojikamua pauni milioni  30.8 kumsajili   Berbatov akitokea Tottenham  mwaka  2008.
Kabla ya kuitema Tottenhm, Berbatov alishafunga mabao  46  katika mechi  102 alizoichezea Spurs.

Hata hivyo hadi anaondoka kwenye klabu hiyo ya  Old Trafford, raia huyo  Bulgaria hakuweza kulipa kile ambacho,  Sir Alex Ferguson alikitarajia kwani baada ya miaka minne aliyoichezea  Manchester United na kisha  kwenda  kujiunga na Fulham, aliuzwa kwa pauni milioni 25, jambo ambalo lilikuwa ni hasara kwa mashetani hao wekundu.

7. Eden Hazard: Lille kwenda  Chelsea –kwa pauni milioni 32

Hazard


Eden Hazard alidhihirisha  mwenyewe kuwa ni kinda mwenye  kipaji Ulaya wakati wa msimu wa  2011-12, hali ambayo ilimfanya  awindwe na timu kubwa kama vile  Chelsea, Manchester United na Manchester City.
Hata hivyo ilikuwa ni Chelsea ambayo ilishinda mbio za kumfukuzia mchezaji huyo wa timu ya Taifa ya Ubelgiji baada ya mchezaji mwenyewe kuamua kujiunga na klabu hiyo wakati timu mbili za Manchester nazo kuwa zimeshakubaliana ada na timu ya Lille ili ziweze kunasa saini yake.

Katika msimu wake wa kwanza, Hazard ameshaanza kufurahia maisha ndani ya klabu hiyo ya jijini London, baada ya kufunga mabao 13 na kutoa msaada wa kupatikana mengine 25 yaliyoisaidia pia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi ya Europa mbele ya Benfica.

 6. Robinho: Real Madrid kwenda  Manchester City – kwa pauni milioni 32

Robinho  aliweka rekodi ya ya kusajiliwa kwa bei mbaya alipotua  Manchester City akitokea Real Madrid  wakati wa usajili wa majira ya joto ya mwaka  2008, chini ya uongozi wa kocha  Mark Hughes.
Baada ya kutua katika timu hiyo, Mbrazil huyo alianza vyema maisha yake na Manchester City, lakini muda mfupi akaanza kuonekana hatayaweza kuyamudu maisha ya michuano ya Ligi Kuu.

Baada ya kutokea hali hiyo, Robinho alipelekwa kukipiga kwa mkopo kwenye timu ya  Santos, ikiwa ni msimu mmoja tu tangu aishi na timu hiyo ya Sky Blues, kabla ya mwaka 2010 kupata kibarua cha kudumu kwenye timu ya  AC Milan.




5. Fernandinho: Shakhtar Donetsk kwenda  Manchester City – kwa pauni milioni 34


Fernandinho amewasili  Manchester City majira haya ya joto  ukiwa ni usajili wa kwanza kwa kocha mpya wa timu hiyo, Manuel Pellegrini, ambaye   amejiunga na  timu hiyo msimu huu, baada ya kuondoka aliyekuwa kocha wa timu hiyo,  Roberto Mancini.

Mchezaji  huyo mwenye umri wa miaka 28, ambaye pia anakipiga kwenye timu ya Taifa ya Brazil, msimu uliopita alifanya vizuri akiwa na timu ya  Shakhtar Donetsk, wakati wa michuano ya Klabu Bingwa Ulaya ya msimu uliopita na hivyo Man City wana matumaini ataendelea na moto huo.

Hadi anaondoka katika timu hiyo ya  Shakhtar Donetsk,  Fernandinho ameichezea   mechi 284 ndani ya kipindi cha miaka nane aliyoishi  Donetsk, na katika kipindi hicho aliweza kupachika mabao kwenye misimu sita.

4. Andy Carroll: Newcastle kwenda  Liverpool –kwa pauni 35

Andy Carroll alisajili kwa gharama iliyovunja rekodi ya usajili Liverpool, ikiwa ni baada ya kuondoka nyota wake, Fernando Torres, lakini naye ameshindwa kuonesha kilichotarajiwa na klabu huyo ya Anfield.
Tangu alipojiunga na timu hiyo, Carroll aliweza kufunga mabao 11 katika mechi  58 alizoichezea Liverpool,  kabla ya kujiunga kwa mkopo na timu ya  West Ham ambako amepewa mkataba wa kudumu wa kuitumikia klabu hiyo ya  Upton Park.

3. Sergio Aguero: Atletico Madrid  kwenda  Manchester City kwa pauni milioni  38

Sergio Aguero alionesha uwezo wake  Manchester City  baada ya kuitema klabu yake ya  Atletico Madrid, muda mfupi kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili la mwaka 2011.

Msimu huo wa kwanza ulikuwa wa manufaa kwa  Aguero, ambapo ilishuhudiwa akiumaliza kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu  akiwa  na Manchester City.

Katika msimu wake wa kwanza, Aguero aliweza kufunga mabao 30 katika mashindano yote na msimu  wa 2012-2013 akaongeza mengine 17.


2. Carlos Tevez: Manchester United kwenda  Manchester City kwa pauni milioni 47


Uhamisho wenye utata wa mmiliki wa mchezaji, Carlos Tevez wa kutoka Manchester United kwenda  Manchester City bado unadaiwa na wengi kuwa gharama hiyo  ya pauni milioni 47 ingekuwa ya  Blues.
Tevez alijiunga na Manchester United akitokea West Ham na akaiwezesha kutwaa ubingwa mara mbili katika kipindi cha miaka miwili aliyoitumikia klabu hiyo ya Old Trafford.
Mchezaji huyo wa timu ya Taifa ya Brazil vilevile aliweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu akiwa na Manchester City, baada ya  kutoka kwenye mgomo kabla ya kuondoka na kujiunga na vinara wa soka Italia timu ya Juventus.

 
1. Fernando Torres: Liverpool  kwenda  Chelsea – kwa pauni milioni 50
Fernando Torres alijinadi mwenyewe  kuwa ni mshambuliaji tishio duniani wakati akikipiga kwenye klabu hiyo ya  Anfield, lakini mchezaji huyo raia wa Hispania ameshindwa kuonesha uwezo wake aliokuwa nao kwenye fulana ya Liverpool tangu atue  Chelsea.
Torres aliwahi kufunga mabao ya haraka  50   kuliko mchezaji yoyote katika historia ya  Liverpool jambo ambalo lilimfanya aingizwe kwenye vitabu vya kumbukumbu za klabu hiyo.

Hata hivyo, hadi sasa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 ameshafunga mabao 15 katika  Ligi Kuu.

No comments:

Post a Comment