Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Sunday, August 11, 2013

GARETH BALE: NI MCHEZAJI KUTOKA SAYARI GANI?


WAINGEREZA huwa wanapenda kujipendelea mno. Wanajua  'kuvifagilia' vitu vyao. Wakitaka kitu fulani kiwe kama wanavyotaka wanaweza. Wanaweza kuiaminisha dunia kwamba kitu fulani kiko hivi kumbe sivyo.
Mlolongo wa ushahidi kuhusu hilo ni mrefu mno kiasi kwamba kama tukiandika makala, kurasa zote za gazeti hili haziwezi kutosha.

Lakini mifano michache katika soka ipo. Mwanzoni kabisa mwa miaka ya tisini, Waingereza walijaribu kuuaminisha ulimwengu wa soka kwamba kiungo wa Manchester United na timu ya taifa ya England wakati huo, David Beckham, ana thamani kubwa kuliko mchezaji yeyote duniani.
Vyombo vya habari vya nchi hiyo vilikuwa vikimpamba kila siku. Dunia iliamini hivyo, ingawa ukweli halisi ni kwamba kipindi hicho kulikuwa na wachezaji wengine wakali zaidi yake.

Ni nani anabisha kwamba Ronaldo de Lima, Rivaldo, Luis Figo, Zinedine Zidane au Ronaldinho hawakuwa juu ya Beckham wakati huo?
Nyota ya Beckham iling'arishwa ikang'ara kisawasawa, hata kama hakufanikiwa kutwaa tuzo yoyote ya mchezaji bora duniani. Hakuambulia hata nafasi ya tatu hadi mwaka 2001 alipofurukuta na kushika nafasi ya pili nyuma ya Luis Figo.

Na kwa mshangao wa wengi, baada ya kuhamia nchini Hispania na baadaye kukutana na Cristiano Ronaldo kwenye kikosi kimoja, alimshangaza nyota huyo wa Ureno baada ya kwenda katika ziara ya bara la Asia, ambako licha ya Ronaldo kuwa juu, lakini mashabiki wengi walikuwa wakimzunguka Beckham kwa sababu waliaminishwa kuwa ndiye supa staa.
Kizazi cha Beckham kikapita, vyombo vya habari vya Uingereza vikateua mchezaji mwingine wa kumpaisha. Ikawa sasa ni zamu ya Michael Owen, ambaye hata hivyo soka yake iliathiriwa kwa kiasi kikubwa na kuwa majeruhi.

Lakini baada ya jina la Owen kufifia, ndipo tulipolazimishwa kuamini kwamba Wayne Rooney ndiye mkali zaidi baada yake, ingawa kiwango chake cha uchezaji ni cha kawaida kabisa.
Lakini kali zaidi ni ya miaka ya hivi karibuni. Kwa misimu miwili iliyopita mshambuliaji wa Tottenham Hotspurs, Gareth Bale, amekuwa miongoni mwa wanasoka nyota na anayewindwa na klabu kubwa barani Ulaya kwa udi na uvumba, na msimu umegeuka kuwa taswira muhimu sana kwa mustakabali wake na klabu yake hiyo.

Baada ya kuonesha kiwango cha hali ya juu msimu uliopita, thamani yake imeongezeka maradufu, lakini pia kiwango cha Bale kilitosha kabisa kuifanya Tottenham kuwa moja ya timu imara zaidi msimu uliopita katika ligi kuu ya England kiasi cha kuiandikia historia timu hiyo kwa kukusanya point 71, zikiwa nyingi zaidi kuweza kukusanywa na timu hiyo kwa msimu mmoja katika historia ya klabu hiyo.
Kwa siku za hivi karibuni, Bale amekuwa gumzo kubwa barani Ulaya na duniani kote, hasa baada ya klabu ya Real Madrid ya Hispania, kuweka bayana nia yake ya kutaka kumsajili mchezaji huyo kwa gharama ambayo itakuwa ni rekodi ya dunia.

Licha ya Madrid kuwa tayari kumnunua mchezaji huyo kwa kitita cha Pauni milioni 85, bado klabu yake ya Spurs, inaona kiwango hicho ni kidogo kulingana na uwezo wa mchezaji mwenyewe.

 Binafsi Bale amekuwa akifurahia na kutaka kujiunga na Real Madrid, ingawa inasemekana kwamba baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo ya Hispania wameanza kununa kwa vile ataonekana kama amewafunika.
Hakuna ubishi, Bale amegubika uhamisho wa kiangazi mwaka huu, kutokana na dau linalovunja rekodi ya dunia lililowekwa mezani na Madrid kumng’oa Tottenham kwenda Santiago Bernabeu, jijini Madrid.
Hadi kufikia jana Jumapili, hatima ya nyota huyo ilikuwa bado haijaamuliwa na pande zote zilikuwa zikiendelea kuvutana, huku muda zaidi wa kuamua kuhusu sakata hilo ili kupisha harakati nyingine, ukiwa unasubiriwa.

Mmiliki wa Tottenham, Joe Lewis, alikuwa akisubiriwa kuamua juu ya sakata la nyota huyo wa kimataifa wa Wales kwenda Madrid, ingawa alikiri hayuko tayari kubariki mauzo chini ya pauni milioni 100.
Lewis, bilionea mkazi wa Bahamas, alikaa meza moja na Rais wa Madrid, Florentino Perez jijini Miami au Phoenix, wakiwa na Mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy, kusaka suluhu kwa faida ya pande zote, kikao ambacho hakikuzaa matunda.

Kiufundi hakuna anayebisha kuwa Bale ni mchezaji mahiri sana ambaye huwa bora zaidi anapocheza kwenye timu inayompa fursa na uhuru wa kucheza kwa kumtengenezea nafasi na pasi nyingi anapokuwa uwanjani, kama alivyokuwa Christiano Ronaldo alipokuwa Man United.
Ukiangalia timu yake ya Tottenham kwa msimu uliopita ilikuwa ikicheza kwa kuhakikisha mchezaji huyo ndio shabaha ya kila shambulio la timu hiyo katika mchezo husika.

Tofauti na Spurs, Bale akijiunga na Madrid ambako atakuwa na Ronaldo kwenye timu, hali itakuwa tofauti, kwani atalazimika kuwa nyuma ya Ronaldo kwa maana ule uhuru wa kuwa kitovu cha mashambulizi ya timu kama alivyokuwa Tottenham, utapotea kwa sababu akiwa Madrid atalazimika kushambulia na kuzuia, hali ambayo ni wazi itaondoa kama si kupunguza makali aliyoonesha msimu uliopita akiwa na Spurs.
Ni rahisi sana kusahau kwamba Bale bado ni kijana mbichi wa miaka 24. Msimu uliopita mshambuliaji huyo alitwaa tuzo mbili za mchezaji bora wa msimu nchini England, lakini pia alitwaa tuzo ya mwanasoka chipukizi wa mwaka.

Ukimuangalia Bale leo huwezi kuamini kuwa huyu ndio mchezaji ambaye alijiunga na Tottenham na kucheza takribani mechi 24 bila ya timu hiyo kushinda hata mchezo mmoja. Lakini mara baada ya hapo mshambuliaji huyo ambaye awali alikuwa beki wa kushoto, kiwango chake kiliimarika kadri siku zilivyosonga na hatimaye msimu uliopita ulidhihirisha kuwa sasa mchezaji huyo ni miongoni mwa wanasoka watatu bora zaidi duniani, akiwa kwenye kiwango cha kina Messi na Ronaldo. Lakini swali la kujiuliza ni kwamba je, kwa dau la Pauni zaidi ya milioni 100 anazouzwa, Waingereza wanataka kutuaminisha kwamba anatokea mwezini au katika sayari nyingine?

No comments:

Post a Comment