MAONESHO YA JUA KALI KIGALI:Ubora na Ubunifu wa Bidhaa za Wajasiriamali wa Tanzania wakosha



Bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wa Tanzania zimeendelea kuvutia maelfu ya wananchi na wageni wanaotembelea Maonesho ya 26 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati, maarufu kama Juakali/Nguvukazi, yanayoendelea jijini Kigali, nchini Rwanda.

Bidhaa hizo zimeonesha ubunifu na uwezo wa wajasiriamali wa Tanzania kuongeza thamani ya mazao ya kilimo cha bustani, yakiwemo matunda na mbogamboga, pamoja na bidhaa za ngozi na mavazi, hali inayoashiria fursa ya kipekee ya kukuza ushindani wa bidhaa za ndani katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Tanzania (Tanzania Day), yaliyofanyika Novemba 6, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu (Mb.), amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wajasiriamali wadogo ili waweze kukuza biashara zao, kuingia katika sekta rasmi na hatimaye kuwa wajasiriamali wakubwa watakaoshiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

 “Nimepata fursa ya kutembelea baadhi ya mabanda ya maonesho na nimefurahishwa kuona bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wajasiriamali wetu. Kwa kweli, bidhaa hizi zinaonesha kuwa wajasiriamali wetu wana ubunifu na uwezo wa kufanya mambo makubwa zaidi iwapo watapewa fursa na mazingira yanayowawezesha,” amesema Mhe. Sangu.




Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kushughulikia changamoto zinazokabili sekta isiyo rasmi, ambazo zimekuwa zikikwamisha ukuaji wa biashara na juhudi za kurasimisha shughuli za wajasiriamali.

Miongoni mwa changamoto hizo ni upatikanaji wa mitaji kutokana na masharti magumu ya mikopo katika taasisi za fedha, ukosefu wa maeneo ya kufanyia shughuli za uzalishaji, changamoto za upatikanaji wa masoko, uelewa mdogo wa masuala ya ujasiriamali pamoja na mazingira duni ya kazi yasiyozingatia staha.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Forodha, Biashara na Fedha, Bi. Annette Mutaawe Ssemuwemba, amesema Jumuiya itaendelea kuunga mkono juhudi za kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati ili kukuza uwezo wao wa uzalishaji, biashara na kipato.

Amesema Sekretarieti ya EAC itaendelea kushirikiana na nchi wanachama katika kuondoa vikwazo vya biashara na kuboresha mazingira ya biashara ya kikanda ili kuwezesha bidhaa zinazozalishwa ndani ya Jumuiya kupata masoko mapana zaidi.

Maonesho hayo yanayofanyika kila mwaka kwa utaratibu wa kupokezana kati ya nchi wanachama wa EAC yamewashirikisha wajasiriamali 364 kutoka Tanzania, ambapo mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Kuendeleza Mnyororo wa Thamani katika Sekta ya Ngozi na Kilimo cha Bustani (Matunda na Mbogamboga) katika Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.” 

 

 

 

 


No comments