TANZANIA MWENYEJI WA MKUTANO WA KIMATAIFA WA UFUGAJI VIUMBE MAJI DESEMBA 2026



Serikali ya Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa Ufugaji Viumbe Maji (International Aquaculture Conference) utakaofanyika Desemba 1 hadi 4, 2026, jijini Dar es Salaam. 

Hayo yameelezwa na Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Maduhu Kazi, wakati akifungua Kikao cha Tano cha Kamati Elekezi ya Programu ya Uchumi wa Buluu ya Umoja wa Ulaya, jijini Dar es Salaam, Novemba 12, 2026.

Dkt. Kazi amesema Uchumi wa Buluu ni fursa muhimu kwa maendeleo ya taifa kutokana na uwezo wake wa kuzalisha ajira, kuvutia uwekezaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuboresha maisha ya wananchi, hususan wanaoishi katika maeneo ya pwani.

Amesema Serikali inaendelea kuimarisha sekta hiyo kupitia majukwaa ya kitaifa na kimataifa, ikiwemo Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Uchumi wa Buluu (IBEC) na Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Aidha, amesema Tanzania iliendelea kuonesha dhamira yake ya kulinda mazingira ya bahari na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia ushiriki wake katika Mkutano wa 11 wa Our Ocean uliofanyika Mombasa, Kenya, Juni 2026.

Akizungumzia programu hiyo, Dkt. Kazi amesema ina uwekezaji wa Euro milioni 110 kutoka Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wake, ikiwa na lengo la kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali za bahari na pwani, kukuza ajira na kuboresha maisha ya jamii zinazotegemea rasilimali hizo.

Amesema tangu kuanza kwa utekelezaji wake, Euro milioni 15.5 zimetolewa kupitia ufadhili wa moja kwa moja wa sekta, huku miradi mitano ya ziada ikiwa imeingia mikataba yenye thamani ya Euro milioni 40.25. Miradi mingine yenye thamani ya Euro milioni 32.6 ipo katika hatua mbalimbali za maandalizi.

Amehimiza washirika wa utekelezaji kuongeza kasi ya shughuli zao ili kuhakikisha fedha zilizotengwa zinageuka kuwa matokeo halisi kwa wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, Umoja wa Ulaya na wadau wengine wa maendeleo.

Aidha, ametoa shukrani kwa Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wake kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maendeleo endelevu, akisisitiza kuwa uratibu wa taasisi, upashanaji wa taarifa na uwajibikaji ni muhimu katika kuhakikisha mafanikio ya programu hiyo.

Programu hiyo inatekelezwa kupitia maeneo matatu makuu ambayo ni usimamizi endelevu wa mifumo ya ikolojia ya bahari na pwani, kukuza biashara za Uchumi wa Buluu zinazozalisha ajira pamoja na kuimarisha mifumo ya utawala na sera.

Miradi inayotekelezwa ni pamoja na LoCAL kupitia UNCDF, Pwani Yetu na Stawi Bluu kupitia GIZ, pamoja na Bahari Yetu kupitia IUCN. Miradi hiyo inalenga kuimarisha uhifadhi wa mazingira, ustahimilivu wa jamii dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kukuza shughuli za kiuchumi zinazotokana na rasilimali za bahari.

Kupitia mradi wa Bahari Yetu, wanafunzi 28 wamepata ufadhili wa masomo ya juu katika vyuo vikuu nchini, wakiwemo saba wa Shahada ya Uzamivu (PhD) na 21 wa Shahada ya Uzamili (MSc).

Vilevile, kupitia mradi wa LoCAL, wilaya tano za pwani ambazo ni Mkinga, Kigamboni, Mafia, Mtama na Mtwara zimehusishwa katika juhudi za kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuandaa miradi ya uwekezaji himilivu.

Katika upande wa upatikanaji wa mitaji, taarifa ya programu imeonesha kuwa kupitia Benki ya CRDB, mikopo ya Uchumi wa Buluu yenye thamani ya Euro milioni 18 imetolewa kwa wateja 988 katika kipindi cha mwaka 2023 hadi 2026, ambapo 925 wametoka Zanzibar na 63 Tanzania Bara.

Kikao hicho pia kimejadili masuala ya uhifadhi wa mazingira ya bahari na pwani, ushiriki wa jamii katika shughuli za uhifadhi, upatikanaji wa fedha endelevu, pamoja na kuimarisha biashara za ufugaji viumbe maji na kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na rasilimali za bahari.

Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Kazi amehimiza washiriki kufanya majadiliano yenye kujenga na kulenga kutatua changamoto za utekelezaji, akisisitiza kuwa uwekezaji unaofanyika unapaswa kuleta manufaa kwa wananchi na kuhakikisha rasilimali za bahari na pwani zinalindwa kwa vizazi vijavyo.

 

No comments