LISSU JELA MIAKA MINNE KWA UCHOCHEZI

 



MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam imemhukumu Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu kifungo cha miaka minne jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la uchochezi.

Hukumu hiyo ilitolewa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akisaidiwa na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Ndunguru alisema mahakama imeridhika kuwa ushahidi wa upande wa mashitaka umethibitisha kosa la uchochezi badala ya uhaini lililokuwa likimkabili mshitakiwa.

Alisema kauli zilizotolewa na Lissu katika mkutano wake zilikuwa na viashiria vya uchochezi na zilichangia kutokea kwa vitendo vya uvunjifu wa amani katika mazingira yaliyolenga kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

“Mahakama imeridhika kwamba kwa mujibu wa Kifungu cha 309 cha Kanuni ya Adhabu, Tundu Lissu ametenda kosa la uchochezi na inamtia hatiani kwa kosa hilo,” alisema Jaji Ndunguru.

Mahakama ilieleza kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha pasipo kuacha shaka ya msingi kuwa Lissu ndiye aliyechapisha na kusambaza video ya hotuba yake ya Aprili 3, 2025 kupitia televisheni ya mtandaoni ya Jambo TV.

Jaji Ndunguru alisema kosa la uhaini lilihitaji kuthibitishwa kwa vipengele vitatu, ikiwamo nia ya kuitisha serikali na kudhihirisha nia hiyo kwa maandishi, machapisho au vitendo vinavyoonekana.

Hata hivyo, mahakama ilibaini kuwa vipengele viwili vya mwisho havikuthibitishwa.

Jaji Ndunguru alisema ushahidi ulionesha kuwa Jambo TV na vyombo vingine vya habari vilivyotajwa ndivyo vilivyorekodi na kusambaza hotuba hiyo.

Pia, upande wa mashitaka haukuthibitisha kuwa Lissu alikuwa na uwezo wa kiufundi kuingia kwenye ukurasa wa kituo hicho na kupakia video hiyo.

Alisisitiza kuwa kutoa hotuba mbele ya waandishi wa habari hakuthibitisha moja kwa moja kuwa mzungumzaji ndiye aliyeisambaza.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga uliomba mahakama kutoa adhabu kali, ukisema kosa hilo ni kubwa na linaweza kuathiri amani na usalama wa taifa.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Lissu alishitakiwa kwa uhaini kwa madai ya kuitisha serikali na kushawishi wananchi kuvuruga Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kwa kusambaza video ya hotuba yake iliyowataka wananchi kutoshiriki uchaguzi huo kupitia Kaulimbiu ya CHADEMA, “No Reforms, No Election”.

No comments