BANDARI ZA ZIWA TANGANYIKA ZAVUKA LENGO


Bandari za Tanganyika zimevuka lengo la kuhudumia shehena katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, baada ya kuhudumia jumla ya tani 236,000 kuanzia mwezi Julai hadi Septemba 2026, sawa na ongezeko la tani 19,000 au asilimia 8.76 ikilinganishwa na tani 217,000 zilizohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2025/2026.

Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw. Plasduce Mbossa, Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Bi. Joyceline Sima, amesema ongezeko hilo ni matokeo ya uwekezaji mkubwa unaotekelezwa na Serikali katika kuboresha na kuimarisha miundombinu ya Bandari za Ziwa Tanganyika.

Ameeleza kuwa maboresho hayo yamekuwa chachu ya kuongeza ufanisi katika shughuli za upokeaji na uhudumiaji wa shehena, huku yakiimarisha uwezo wa bandari kuhudumia wateja na wafanyabiashara kwa ufanisi zaidi.



Bi. Sima amesisitiza kuwa uwekezaji unaoendelea katika miundombinu ya bandari una mchango mkubwa katika kuongeza uwezo wa kiutendaji, kukuza shughuli za biashara na kuimarisha mchango wa Bandari ya Kigoma katika kukuza uchumi na biashara za ndani na nchi jirani.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inaendelea kuboresha miundombinu na huduma za bandari nchini kwa lengo la kuongeza ufanisi, ushindani na kuchochea ukuaji wa uchumi.

No comments